December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbunge Viti Maalumu aidai Wizara mambo 3

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dodoma

MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Rukwa kwa tiketi ya CCM, Bupe Mwakang’ata ameishauri Serikali mambo matatu muhimu ikiwa ni pamoja na kuharakisha malipo ya wakandarasi nchini ambao wanaidai Serikali baada ya kukamilisha ujenzi wa miundombinu nchini.

Aidha, Mwakang’ata ameiomba Serikali kuanza ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga Mjini na ujenzi wa kiwango cha lami barabara inayoanzia Kibaoni hadi Mlowo ikiunganisha mikoa minne. Mikoa hiyo ni Rukwa, Katavi, Songwe na Mbeya.

Mwakanga’ata aliomba mambo hayo alipokuwa akichangia mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi wakati wa Mkutano wa Tatu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kikao cha 30 jijini Dodoma Mei 18, 2021.

Mbunge huyo, alianza mchango wake katika wizara hiyo akiipongeza waziri na naibu waziri kwa kazi kubwa ya kuunganisha barabara za Tanzania kwa lami.

Hata hivyo, alisema katika hoja zake za msingi, pamoja na kazi nzuri ambayo Serikali inafanya, lakini kuna changamoto ya wakandarasi, ambapo wanalalamika sana kwa kucheleweshewe malipo yao wanapokuwa wamefanyakazi.

Lakini pia, alisema wakifanyakazi kabla ya kulipwa, wanakatwa fedha zao kwenye akaunti zao na kufungiwa bila utaratibu.

“Mheshimiwa Spika, hilo Wizara iliangalie kwa makini na ilifanyie kazi, wakandarasi wetu ni wazalendo na ni Watanzania wamefanyakazi nzuri ya kuhakikisha barabara zetu ni nzuri pamoja na changamoto ya mvua,” alisema Mwakang’ata.

“Eneo lingine ambalo mbunge huyo alizungumzia ni Uwanja wa Ndege wa Mkoa wa Rukwa, Sumbawana Mji.

Alisema uwanja huo umezungumziwa sana zaidi ya miaka minne wanapopitisha bajeti,lakini matokeo ni hakuna kinachoendelea.

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Rukwa, akichangia mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi bungeni Dodoma, ambapo ameiomba Serikali kujenga Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga pia aliishauri Serikali kuwalipa wakandarasi madai yao ya muda mrefu.

“Tunaishukuru Serikali mwaka juzi imeweza kuwalipa watu waliokuwa wanauzunguka uwanja huo mdogo wa zamani, lakini baada ya hapo hakuna kinachondelea, wakati Mkoa wa Rukwa ni kivutio cha utalii mbalimbali, utalii wa Maporomoko wa Karambo Force, utalii wa wanyama, kuna madini ya kutosha, lakini kuna wafanyabiashara wa mazao,” alisema Mwakang’ata na kuongeza;

“Kuna wafanyabiashara wakubwa ambao wangeweza kutumia usafiri wa ndege kuja Dar es Salaam, kwenda Dodoma na kurudi Sumbawanga.”

Aliomba Waziri wakati wa kutoa majumuisho ya michango ya wabunge awaeleze uwanja wa ndege wa Sumbawanga Mjini utajengwa lini.

Jambo la tatu ambalo Mbunge Mwakang’ata alizungumzia ni kuhusu barabara, alisema kuna barabara moja ambayo ni uchumi wa mkoa wa Rukwa, Katavi, Songwe na Mbeya.

Alisema barabara hiyo inatoka Kibaoni hadi Mlowo. Kwa mujibu wa mbunge Mwakang’ata barabara hiyo nayo imezungumziwa sana.

“Barabara hii Serikali imekuwa ikitengeneza vipande baada ya muda inaharibika, daraja linahama na Serikali inarudi tena kutengeneza,” alisema.

Aliishauri Serikali kwamba mwarobani wa barabara hiyo ni kuweka lami. Aliongeza kwamba inapopita barabara hiyo ni Bonde la Rukwa, mazao mengi mengi yanalimwa kule, mpunga unalimwa kule, ufuta unapatikana kule na mazao mengine ya kila aina yanapatikana kule.

“Kwa hiyo tunaiomba sana Serikali barabara hii ijengwe kwa kiwango cha lami,” alisema.

Kwa upande wa bandari, alisema mkoa huo una bandari kama tatu, lakini hazifanyi kazi yoyote.

“Serikali imewekeza fedha nyingi za kutosha kwenye bandari hizo, lakini hazifanyi chochote, kwa hivyo alishauri Serikali iweke nguvu kwenye bandari hizo ili ziweze kuingiza pato la Serikali.