April 2, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwakagenda:Zao la ndizi liuzwe katika masoko ya kimataifa

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

MBUNGE wa Viti Maalum Sophia Mwakagenda ameiomba Serikali ione umuhimu wa zao la ndizi kupelekwa katika masoko ya kimataifa Ili wakulima wa zao hilo waweze kunufaika.

Mwakagenda ametoa kauli hiyo wakati akiuliza swali nyongeza Bungeni jijini Dodoma jana huku akitolea mfano wa Nchi za Caribian kwamba zinaishi kwa kutegemea zao la ndizi katika masoko ya kimataifa.

“Je Serikali haioni sasa Kuna haja ya kuhakikisha zao la ndizi linauzwa kimataifa kwa sababu soko bado lipo?”amehoji Mwakagenda

Pia katika swali lake la nyongeza Mbunge huyo alitaka kujua kwa nini Serikali isishushe fedha na ofisi za Shirika la Maendeleo la Viwanda Vidogo (SIDO) hadi wilayani ili iweze kuwasaidia wananchi wa ngazi za chini.

Akijibu maswali hayo Naibu Waziri wa Viwanda Exaud Kigahe amesema amechukua mawazo ya Mbunge huyo huku akisema Serikali inapenda mazao kama ndizi yakauzwe katika masoko ya kimataifa ambapo amesema ,inaendelea kutafuta masoko zaidi ya zao hilo.

Aidha amesema lengo la Serikali ni mazao ya Kilimo kuongezwa thamani ambapo tayari Rais Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa kuongeza bajeti ya Kilimo na uzalishaji umeongezeka hivyo yakiweza kuchakatwa itaongeza thamani kwa wakulima na mnyororo mzima wa mazao katika sekta ya Kilimo na wafanyabiashara kwa ujumla.

Kuhusu SIDO kushushwa ngazi ya wilaya,Naibu Waziri huyo alisema ,lengo la Serikali ,SIDO ishuke hadi ngazi ya Halmashauri huku akisema Waziri wa Viwanda Selemani Jafo alishatoa maelekezo hayo ya kufungua ofisi ngazi za Halmashauri ambapo pia alisema mwaka ujao wa fedha SIDO itaongezewa fedha ili ifanye vizuri zaidi.

Awali katika swali lake la msingi,Mwakagenda alitaka kujua lini Serikali itatafuta Wawekezaji wa Viwanda vidogo vidogo vya kuongeza thamani katika zao la Ndizi.
Akijibu swali hilo Kigahe amesema,mkakati wa Serikali wa kutafuta wawekezaji wa viwanda vidogo ni kupitia utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (MKUMBI) kwa kuwajengea uwezo watanzania ili waanzishe viwanda vidogo.

Pia amesema, Serikali imeendelea kuhamasisha uwekezaji wa viwanda vikubwa vya kuchakata mazao ili kuyaongezea thamani kwa wingi zaidi ikiwemo zao la ndizi.

Kwa mujibu wa Kigahe Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) limeendelea kuwajengea uwezo wajasiriamali wadogo katika maeneo yao kulingana na fursa zinazopatikana huko ili waweze kufanya uwekezaji wa viwanda vidogo vya kuchakata mazao mbalimbali ikiwemo zao la ndizi kwa kuwezesha teknolojia za usindikaji wa Kaukau za Ndizi (Banana Crisps), Mvinyo wa Ndizi, Pombe kali na Unga wa Ndizi.