January 7, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mvua ya upepo yaboma nyumba, watu 11 wajeruhiwa

Na Israel Mwaisaka,TimesMajira Online. Rukwa

NYUMBA 17 zimebomoka huku watu 11, wakijeruhiwa kutokana na mvua kali yenye upepo iliyonyesha juzi katika Kijiji cha China Kata ya Kate wilayani Nkasi huku wengi wakiachwa bila ya makazi.

Akitoa taarifa kwa Mkuu wa Wilaya Nkasi, Said Mtanda aliyetembelea kijiji hicho kujionea maafa yaliyotokea Ofisa Mtendaji wa Kijiji, Conrad Kauzeni amesema mvua hiyo ilianza kunyesha juzi majira ya saa 11 jioni na baada ya muda, ilikuja mvua yenye upepo mkali na kubomoa nyumba hizo huku watu wengine wakijeruhiwa vibaya.

Amesema kutokana na hali hiyo, wananchi walijitokeza kwenda kuwakoa wenzao huku majeruhi wakikimbizwa Kituo cha Afya Kate kwa ajili ya matibabu.

Ofisa Mtendaji huyo, amesema wanamshukuru mwekezaji wa shamba la Msipazi Farm kijijini hapo kwa msaada mkubwa wa kutoa gari kuwakimbiza majeruhi kwenda kituo cha afya, ikiwa ni pamoja na kugharamia matibabu ya waathirika hao.