Na Grace Gurisha, TimesMajira Online, DSM
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi maarufu kama Mahakama ya Mafisadi, imemuhukumu mfanyabiashara Ayoub Kiboko na mke wake Pilly Kiboko kifungo cha miaka 20 gerezani, baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya gramu 251.25 aina ya heroin.
Aidha, Mahakama hiyo imeamuru vielelezo ambavyo ni dawa za kulevya viteketezwe, huku vielelezo vingine ambavyo ni magari matatu yarudishwe kwa washtakiwa.
Hukumu hiyo imesomwa leo Desemba 18,2020 na Jaji Mfawidhi, Lilian Mashaka wa Mahakama hiyo, baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi sita wa upande wa mashtaka, upande wa utetezi, vielelezo 16 na sheria na kufikia kutoa hukumu hiyo.
Jaji Mashaka amesema kuwa ushahidi wa upande wa mashtaka umethibitisha kesi kwa mshtakiwa wa kwanza (Kiboko) wa pili (Pilly) hivyo mahakama inawatia hatiani kwa makosa wanayoshitakiwa nayo ya kusafirisha dawa za kulevya.
Amesema kwa maoni yake utetezi wa washtakiwa  uliunga mkono ushahidi wa upande wa mashtaka kutokana na kujichanganya kwa maelezo yao ya ushahidi waliyoutoa Mahakamani hapo.
Mahakama imezingatia sheria za dawa za kulevya na pia tangu washtakiwa wakamatwe Mei 23, 2018 na muda wote, waliokaa gerezani, hivyo imewahukumu kifungo cha miaka 20 jela na kama hawajaridhika wana haki ya kukata rufaa.
Aidha, Jaji Mashaka amesema mshtakiwa wa Kiboko na Pilly walikuwa wanajua kwamba kulikuwa na dawa za kulevya katika sehemu ya kuwekea viatu, kwa hiyo wanahatia kwa kukutwa na dawa hizo.
Baada ya washtakiwa kutiwa hatiani, Jaji Mashaka aliwauliza kama wanachochote cha kusema, ambapo Kiboko aliiomba mahakama isiwape adhabu kali licha ya kutiwa hatiani na pia ni shtaka la kwanza kutenda.
Kwa upande wa Pilly, aliiomba mahakama imuhurumie kwa sababu ana watoto watatu, hajawaona kwa muda mrefu, hivyo mahakama imuonee huruma.
Kesi hiyo kwa upande wa Serikali iliwakilishwa na Wakili wa Serikali, Salim Msemo, Costantine Kakula na Candid Nasua ambao ndiyo waliendesha kesi hiyo hadi inatolewa hukumu na upande wa utetezi alikuwa Majura Magafu.
Katika kesi ya uhujumu uchumi namba 29/2018, Kiboko na Mkewe wanadaiwa, Mei 23, 2018 eneo la Tegeta Nyuki Masaiti, Wilaya ya Kinondoni,  walisafirisha dawa za kuĺevya aina ya heroin zenye uzito wa gramu 251.25
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
27 kulipwa kifuta jasho Nkasi
Mwakilishi Mkazi wa UN nchini awasilisha hati