Fresha Kinasa, TimesMajira Online Mara.
WANAFUNZI waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza Kijiji cha Muhoji Jimbo la Musoma Vijijini Mkoani Mara, wanatarajia kuondokana na changamoto ya kutembea umbali mrefu wa kilometa 10 kwenda masomoni kwenye Sekondari ya Kata iliyoko Kijijini Masinoni kutokana Wananchi wa Kijiji hicho kujenga Sekondari yao.
Hayo yamebainishwa kupitia taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Januari 5, 2025, Ambapo imesema, Muhoji Sekondari ipo tayari mwezi huu kuanza kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza kutoka Kijijini humo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa,Ujenzi wa shule hiyo ulianza kwa kupitia Harambee za Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo,ambae amechangia fedha zake binafsi. Huku Mfuko wa Jimbo ukiwa umechangia baadhi ya vifaa vya ujenzi.
“Wanakijiji wanachangia fedha za ujenzi na nguvukazi zao. Serikali yetu imeanza kuchangia ujenzi wa Sekondari hii kwa kutoa Shilingi Mil.75,tunashukuru Sana, Muhoji Sekondari iko tayari, mwezi huu (Januari 2025) kuanza kupokea wanafunzi wa Kidato cha Kwanza kutoka kijijini humo.”imeeleza sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza.
“Sekondari hii mpya, kwa miaka ya karibuni, itapokea wanafunzi kutoka vijiji jirani vya Kaburabura (Kata ya Bugoji), Saragana (Kata ya Nyambono) na hata wanafunzi kutoka Wilaya ya Bunda, Kitongoji jirani sana cha Kinyambwiga”imeeleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, majengo yaliyokamilishwa ni Vyumba vya madarasa vitatu (3), Ofisi moja, Vyoo matundu 8 wasichana, na 6 wavulana, Chumba cha Maktaba, Chumba cha Huduma ya Kwanza (matibabu).
Aidha, Ujenzi wa miundombinu ya elimu kwenye sekondari hiyo mpya umetajwa kuwa unaendelea, ikiwemo maabara tatu za masomo ya sayasi, vyumba vipya vya madarasa, na nyumba za walimu.
Fabian Augustine ni Mkazi wa Muhoji akizungumza na Majira Online, amepongeza juhudi kubwa zilizofanywa kwa pamoja baina ya Wananchi, Mbunge Pro. Muhongo na Serikali kuhakikisha Sekondari hiyo inatatua changamoto ya umbali mrefu kwa Watoto kwenda Masomoni.
More Stories
Mtoto wa mwaka mmoja na miezi kumi,adaiwa kubakwa na baba wa kambo
Ashikiliwa kwa tuhuma za kusambaza picha akidai anauza mtoto
Tanzania,Italia kushirikiana kuendeleza sekta ya madini