January 2, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mufindi yaonya wazazi watakaotorosha wanafunzi

Na Zuhura Zukheir,TimesMajira Online. Iringa

MKURUGENZI wa Halmashauri ya Mufindi, Nettoh Ndilito ametoa onyo kwa wazazi watakaobainika kuhusika na utorojwaji wa wanafunzi, wanaotarajia kuanza kidato cha kwanza Januari mwakani ambapo amesema anataka kuona wanafunzi wote 665 waliochaguliwa, wanajiunga katika shule watakazopangiwa.

Ameyasema hayo katika Kijiji cha Madilo Kata Mdabulo wilayani Mufindi wakati akizungumza na wananchi waliohudhuria mkutano na uongozi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Mkurugenzi huyo amesema, amepokea taarifa za kuhuzunisha kuwa kuna baadhi watoto wa kike waliohitimu darasa la saba mwaka huu, wameolewa na wengine ni wajawazito.

Amesema kitendo hicho kinamnyima haki mtoto na kumuathiri kisaikolojia kwa kuwa wanaingia katika majukumu wakiwa na umri mdogo, jambo ambalo limekuwa likikemewa vikali na serikali.

Ndilito amesema Halmashauri ya Mufindi, wanafunzi 665 wamechaguliwa kujiunga na sekondari na hatarajii kuona mtoto hata mmoja hajaripoti shuleni.

Kauli hiyo imeungwa mkono na Mwenyekiti wa Kamati ya Miradi Utawala na Fedha ya TASAF, Naftar Ng’ondi ambapo alisema hatarajii kuona watoto waliopo katika mpango wa mfuko huo, wanashindwa kwenda kujiunga kidato cha kwanza kwa namna yoyote ile.

Amesema serikali kupitia TASAF, imekuwa ikitumia fedha nyingi kuhakikisha waliopo katika kaya maskini wanapata mahitaji yote ikiwemo elimu, lishe, pamoja na afya hivyo watoto wote wanatakiwa waende shule.

Ng’ondi amesema kwa upande wa Iringa Vijijini katika Kijiji cha Matembo Kata ya Kising’a, wazazi wamefanya vizuri kwenye usimamizi wa watoto katika elimu ambapo hadi sasa, kuna wanafunzi waliopo shule za msingi, sekondari wengine wapo kidato cha tano na sita huku wengine wakiwa vyuoni.