Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline
KAMA kuna jambo la kutunza na kulindwa kwa wananchi wa mikoa ya Tanga na Kilimanjaro ni Mto Pangani.
Mto huo umeshikilia uhai wa wananchi hao kuanzia shughuli za maendeleo ikiwemo kilimo na uvuvi, huduma za jamii, tamaduni na desturi.
Mto Pangani, pamoja na shughuli za binadamu kuanzia kutumia kwa kilimo, uvuvi, mifugo, matumizi ya nyumbani ikiwemo kunywa na kuoga, pia umekuwa muhimili kwa Serikali hasa katika kufua umeme.
Ikumbukwe, umeme wa kuzalisha kwa kutumia maji kwa nchi ya Tanganyika (sasa Tanzania), ulianza Mto Pangani eneo la Hale, Wilaya ya Korogwe mwaka 1934, kisha mitambo ya kufua umeme kuongezwa maeneo mengine ya nchi ikiwemo Bwawa la Nyumba ya Mungu lililopo Wilaya ya Mwanga, ambalo nalo linategemea maji ya Mto Pangani.
Lakini pamoja na Serikali kuanza kuutumia Mto Pangani kwa kujenga miundombinu ya maji mwaka 1974 kwa ajili ya Wilaya ya Handeni kupitia ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GTZ) na sasa GIZ kwa jitihada za Mbunge wa Jimbo la Handeni kwa wakati huo, Mussa Masomo, bado wananchi wa mikoa ya Tanga na Kilimanjaro waliutumia mto huo tangu dunia kuumbwa, wakitumia maji hayo kwa shughuli mbalimbali.
Mwandishi wa makala haya amezungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Handeni Trunk Main (HTM) Mhandisi Yohana Mgaza, ambaye ameelezea namna wanavyotunza mazingira kwa ajili, pamoja na mambo mengine, ni kuulinda Mto Pangani uwe endelevu kwa ajili ya kuwa chanzo muhimu cha miradi ya maji.
Mhandisi Mgaza ambaye mamlaka yake sasa inahudumia Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Halmashauri ya Mji Handeni, Halmashauri ya Mji Korogwe, na Mamlaka ya Mji Mdogo Mombo uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, wanajua umuhimu wa kutunza mazingira yote yanayouzunguka Mto Pangani ambapo chanzo chake kikuu ni Mlima Kilimanjaro.
“Mto Pangani ni muhimili kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mingi ya maji ya Serikali. Serikali ilianza kutumia Mto Pangani kujenga miundombinu ya maji mwaka 1974 kwa kujenga Mradi wa Maji Handeni Trunk Main. Mradi huu ulikuwa mkombozi kwa wananchi wa wilaya hiyo sababu Wilaya ya Handeni haina mto wa maji yanayotiririka kwa mwaka mzima.
“Lakini bado, Mto Pangani unategemewa kwa asilimia 100 kwa ajili ya Mradi wa Maji wa Miji 28, ambapo Mkoa wa Tanga umeweza kupata miji minne (4) ya Handeni, Korogwe, Muheza na Pangani. Kutokana na umuhimu huo, kila mwaka tunatenga bajeti kwa ajili ya utunzaji mazingira kwa ajili ya vyanzo vyote vya maji ikiwemo Mto Pangani,”anasema Mhandisi Mgaza.
Mhandisi Mgaza anasema ukiacha chanzo cha maji cha Mto Pangani, pia wana vyanzo vingine vya maji ikiwemo Mto Mashindei kutoka Milima ya Usambara eneo la Tarafa ya Bungu, Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, Mto Mbeza uliopo Halmashauri ya Mji Korogwe, na Mto Nkozoe uliopo Kata ya Vuga, wilayani Lushoto.
Lakini pia, wana vyanzo vya maji kupitia visima virefu zaidi ya 15 kwenye Halmashauri ya Mji Korogwe na Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, na Halmashauri ya Mji Handeni. Huko kote ili maji yaweze kuwa endelevu, ni lazima vyanzo vya maji viweze kutunzwa.
“Ipo bajeti ya utunzaji mazingira. Na ili kuwa na mazingira endelevu ambayo yataweza kufanya mtiririko wa maji kuwa endelevu, kuna vikundi vinawezeshwa ili kuweza kulinda mazingira. Vinapewa vitendea kazi na miche ya miti ili viweze kupanda maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye mito, na maeneo ya chemchemi za maji. Miche hiyo tunanunua mmoja sh. 500, lakini tunaponunua miche zaidi ya 100 bei inapunguzwa, hivyo kununua mingi zaidi” anasema Mhandisi Mgaza.
Mhandisi Mgaza anasema eneo la mamlaka yake ni kubwa, hivyo wasipotunza mazingira itawagharimu, sababu kutokana na uchache wa miundombinu ya kuvuta maji bado ni michache, na maeneo mengine ya wilaya ya Handeni na Korogwe wanategemea visima virefu, inabidi kuwe na ushirikiano kati yao na viongozi wa wilaya, halmashauri, tarafa, kata, vijiji, mitaa na vitongoji ili kulinda mazingira.
Anasema kuna visima virefu zaidi ya 15 kwenye wilaya za Handeni na Korogwe, ambavyo vinatoa huduma ya maji kwa asilimia 100 kwa wananchi hao, huku akitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni iliyopo Halmashauri ya Mji Handeni wa Kwamagome na Kwediamba, na Majani Mapana, Halmashauri ya Wilaya ya Handeni.
ATHARI ZA KILIMO NA UFUGAJI
Mhandisi Mgaza anasema moja ya changamoto kwenye Mto Pangani ni shughuli za kilimo na ufugaji wa mifugo holela, kwani baadhi ya wakulima wanadiriki kulima mashsmba hadi mita nne ndani ya Mto Pangani, jambo hilo linahatarisha uhai wa mto huo, kwani kwa kawaida wanatakiwa kulima nje ya mita 60..
Lakini kwa kulima hadi kwenye mto maana yake wanachafua maji hasa mvua inaponyesha sababu maji hayo yanakwenda kuingia kwenye mitambo ya kusukuma maji, hivyo kufanya maji yatakayotoka kwenye mabomba kuwa machafu.
Lakini kuna wanaokata miti kwa ajili ya kuchoma mkaa, watu hao wanakata miti mpaka iliyopo pembezoni mwa mito na vyanzo vingine ikiwemo Mto Pangani. Jambo hilo ni la hatari kwa vile linahatarisha vyanzo vya maji kupungua ama kutokuwa endelevu.
“Kilimo kisichokuwa rasmi na kusafisha mashamba, ufugaji wa kuingiza ng’ombe mtoni na kuchafua maji, kukata miti na kuchoma mkaa na kuni, ni hatari kwa vyanzo vya maji. Mosi, kunasababisha mmomonyoko wa udongo kwenye mito na maji kuchafuka hasa kipindi cha mvua, kupungua kwa maji, na wakati mwingine kukauka kabisa, hasa Mto Mbeza, ambapo mwaka juzi (2022) ulikauka kabisa.
“Lakini kusababisha mgao wa maji kuwa mkali, na wengine kukosa kabisa, na kusababisha malalamiko kwa wananchi kuwa wanakosa maji kumbe chanzo ni wao kuharibu mazingira” anasema Mhandisi Mgaza.
Mhandisi Mgaza anasema wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Mazingira Duniani ya kila Juni 5, viongozi wa Serikali wa ngazi zote na wadau wa maendeleo na mazingira, washirikiane kutunza mazingira ili urithi wa mito, maziwa na bahari iwe endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho.
More Stories
MSF ilivyojidhatiti kusaidia serikali katika utoaji wa huduma za afya
Prof.Muhongo awapongeza vijana 32 waliotembea kwa miguu kutoka Butiama hadi Mwanza
Rais Samia atimiza ahadi Hanang