Na Penina Malundo,TimesMajira Online.
MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania, umempongeza Rais, Samia Suluhu Hassan kwa kutoa agizo kwamba vyombo vya habari vilivyofungiwa vifunguliwe kwani agizo hilo, limeleta matumaini mapya yenye uhai kwa vyombo vya Habari nchini kufanya kazi zake kwa uhuru.
Akitoa taarifa Dar es Salaam Mratibu wa Kitaifa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania, Onesmo Olengurumwa amesema kabla ya agizo la Rais Samia kumekua na hofu kubwa miongoni mwa vyombo vya habari na waandishi wa habari kuhusu uhuru katika kazi zao.
Amesema katika kuhakikisha taifa linaendelea kuwa na vyombo vya habari huru na vyenye mchango katika maendeleo, Mtandao wao kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya habari, umekua ukisaidia kwa namna mbalimbali sekta ya habari.
Olengurumwa amesema miongoni mwa mchango mkubwa wa Mtandao katika sekta hiyo ni kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari, kufanya uchechemuzi ili kupata sheria bora na kutoa msaada wa kisheria kwa waandishi waliopatwa na madhila mbalimbali katika kazi zao ambapo hadi sasa, Mtandao umetoa msaada wa kisheria kwa zaidi
ya waandishi wa habari 50 katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita.
“Mtandao wetu umekua ukishirikiana na wadau mbalimbali wa habari katika kujenga na kudumisha uhuru wa habari baadhi ya wadau hao ni Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEFF), wamiliki wa vyombo vya habari na Baraza la Habari Tanzania (MCT),” amesema.
Amesema wadau wengine ni Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na kazi kubwa zilizofanyika ni uchechemuzi na kuwajengea uwezo waandishi wa habari na vyombo vya habari nchini.
More Stories
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa