Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
SHIRIKA lisilo la kiserikali la MDG (Management and Development for Health) Mkoani Tabora limetoa msaada wa vitendea kazi kwa watoa huduma za afya kwa jamii (CHW) vyenye thamani ya zaidi ya sh mil 27.
Akipokea vifaa hivyo jana Mstahiki Meya wa halmashauri ya manispaa Tabora Ramadhan Kapela amelipongeza Shirika hilo kwa kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya 6 za kuboresha utoaji huduma za afya kwa jamii.
Alisema watoa huduma hao wanafanya kazi nzuri sana ila wamekuwa wakifanya kazi zao katika mazingira magumu, hivyo msaada huo umekuja wakati mwafaka, sasa kazi iliyobaki ni kuboreshwa huduma za afya zinazotolewa kwa jamii.
Alisisitiza kuwa vifaa hivyo (baiskeli 8 na bajaji 3 za kisasa) vinapaswa kutumika kwa kazi iliyokusudiwa na sio vinginevyo, kwani vimeletwa kwa lengo moja tu la kusogeza huduma za afya karibu na walengwa.
‘Ndugu zangu mmepata vitendea kazi, nendeni mkaboreshe huduma zenu, msitumie vifaa hivi kubeba abiria, mkiviharibu mtakuwa mmejiharibia wenyewe, kumbukeni mlivyokuwa mnahangaika kwenda kwa wateja’, alisema.
Kaimu Mkurugenzi wa manispaa hiyo Seif Salum alisema vifaa hivyo ni nyenzo muhimu ya kuboresha huduma za afya kwa wagonjwa wa majumbani hasa wale wenye maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) na wenye kifua kikuu (TB).
Aliomba wadau wengine kujitokeza kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan za kujenga zahanati, vituo vya afya na hospitali za wilaya ikiwemo manunuzi ya vifaa tiba ili kuboresha huduma za afya kwa jamii.
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa ya Tabora Dkt Pascal Matagi alisema basikeli 8 zimegharimu kiasi cha sh 1,920,000/- na bajaji 3 za kisasa zenye matairi 4 zimegharimu sh 25,500,000.
Aliongeza kuwa baiskeli zitagawiwa katika zahanati za kata ya Ikomwa (Ikomwa), Misha (Itaga), Itonjanda (Manoleo), Ndevelwa (Ndevelwa), Ipuli (St Anna), Ng’ambo (St Filipo), Tumbi (Tumbi) na Kakola (Kakola).
Alisisitiza kuwa bajaji zimetolewa kwa Hospitali ya Rufaa Kitete, Zahanati ya Town Clinic (Chemchem) na Zahanati ya Cheyo, ili kuwarahisishia utoaji huduma watoa huduma za afya ya jamii wa majumbani.
Mratibu wa Shirika la MDH, Daktari Agness Maduka alisema wametoa vifaa hivyo ili kuboresha utoaji huduma kwa wagonjwa walioko majumbani haswa walio na maambukizi wa TB na VVU.
Alisema ili kuwaongezea ufanisi watoa huduma (CHW) watakuwa wanatoa mafuta ya bajaji hizo na kuzifanyia matengenezo punde zinapoharibika, hivyo akawataka kuzitumia kwa kazi iliyokususiwa huku akitahadharisha kuwa zimefungwa kifaa maalumu cha kuona kila kinachofanyika.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua