December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Msomera wapokea vifaa vya TEHAMA

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline.

MFUKO wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF)umeeleza utekelezaji wa majukumu yake na kazi ambayo imefanya ya kuboresha mawasiliano nchini ikiwemo kupeleka vifaa vya TEHAMA katika kijiji cha Msomera.

Akizungumzia utekelezaji huo Mtendaji Mkuu wa UCSAF,Justina Mashiba amesema kuwa wao wanakwenda katika maeneo magumu kufikika hivyo serikali ilivyoamua kuwatoa wananchi wanaoishi Ngorongoro na kuwapeleka katika kijiji cha Msomera ambacho kipo katika Wilaya ya Handeni wao kama UCSAF wamefanya miradi mitatu katika eneo hilo.

“Kwanza tumejenga mnara katika kijiji cha Msomera kwa kushirikiana na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) ambao ndiyo wamejenga mnara huo,lakini tunawashukuru watoa huduma wote wa mawasiliano kwa sababu wote wamepeleka huduma zao huko kupitia ule mnara na wao wameweza kwenda kuweka vifaa vyao pale na hivyo basi eneo lile la Msomera usikivu wa mitandao yote unapatikana tunashukuru kwzi hizo ni juhudi za Serikali kupitia kupitia UCSAF,”amesema Mashiba.

Hata hivyo amesema kuwa wakiwa ziarani Wilayani Handeni na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye waliambiwa kuwa kuna ujenzi wa nyumba nyingine takribani 5000 kwajili ya wananchi kutoka Ngorongoro kuhamia tena katika eneo hilo la Msomera lakini kwasasa ni kwenye kijiji kinaitwa Mkababu.

Mashiba amesema kuwa ilionekana katika kijiji hicho kunachangamoto ya mawasiliano kwasababu ni eneo ambalo hakuna mtanzania aliyekuwa anaishi hapo lakini kwa sasa kuna watu wanakuja hivyo wao kama UCSAF na jukumu lao kuhakikisha wanapeleka huduma za mawasiliano kwa kushirikiana na TTCL kwenda kupeleka huduma za mawasiliano eneo hilo.

“Mradi upo katika hatua za mwisho na utakamilika kabla hata ya wale watanzania hawajahamia kwahiyo watakapofika moja kwa moja watakuta kwamba huduma za mawasiliano zipo vizuri kabisa katika eneo hilo na niseme katika eneo lile la Msomera huduma zinazopatikana ni 4G,”amesema Mashiba.

Aidha ameeleza kuwa UCSAF haiendi tu kwenye huduma za mawasiliano bali wanatumia pia TEHAMA kuweza kuhakikisha wanafunzi au jamii kwa ujumla wanaweza kupata elimu ya TEHAMA kwa kupitia vifaa mbalimbali vya TEHAMA.

“Shule ya msingi Samia Suluhu ni shule moja wapo ya mfano ya wanufaika wa mradi wa kupeleka vifaa vya TEHAMA kwenye shule zetu za umma na tumepeleka kompyuta katika darasa lile,tumepeleka projecta na printa lakini vilevile tumeshirikiana na wenzetu wa TTCL tumepeleka mkongo wa Taifa katika eneo hili na shule hiyo wanadarasa zuri la TEHAMA wanaofundisha watoto wale waliotoka katika jamii ya kimasai waweze kupata taarifa mbalimbali kupitia TEHAMA,”amesema Mashiba.

Pamoja na hayo Mashiba ameeleza kuwa upatukanaji wa huduma ya mawasiliano mpaka sasa wamesaini mikataba yakupeleka huduma za mawasiliano katika kata zaidi ya 1900 kwa kufanya hivyo mradi huo ukikamilika ambao kwa sasa upo kwenye asilimia 90 kwahiyo imebaki asilimia 10 tu watakuwa wamemaliza ujenzi wa minara katika maeneo hayo yote na watakavyokamilisha watanzania wapatao milioni 15 watapata huduma za mawasiliano kupitia ushirikiano au kupitia serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Niwashukuru watoa huduma wote za mawasiliano ambao ndiyo tunashirikiana nao na mara zote ninasema ushirikiano huu wa mfuko wa mawasiliano kwa wote pamoja na watoa huduma za mawasiliano kwa wote pamoja na watoa huduma za mawasiliano ni moja ya mifano mizuri ya mahusiano kati ya serikali na sekta binafsi pamoja na serikali huu ni mfano ambao uko hai kabisa,”amesema Mashiba.