Na Mwandishi Wetu,Timesmajira
Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Wakala ya Serikali Mtandao (e-GA) inaendelea na hatua za mwisho za ukamilishaji wa ujenzi wa mfumo wa Usajili na utoaji wa vitambulisho vya kidigitali kwa Waandishi wa Habari nchi nzima – Journalists Accreditation & Registrations System (JARS).
Mfumo huo unaotengenezwa na chini ya Idara ya Habari (Maelezo) na Wataalamu wa Mifumo wa e- GA, unalenga kurahisisha, kuongeza uwazi na kuimarisha utendaji kazi wa waandishi wa Habari kwa kuwapatia huduma ya usajili na utoaji wa vitambulisho vya kazi katika maeneo yao bila kulazimika kusafiri kwenda Dodoma au Dar es salaam kupata huduma hiyo.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na Msemaji Mkuu wa Serikali,Gerson Msigwa wakati akitoa taarifa kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo miradi iliyotekelezwa na serikali ya awamu ya sita wakati wa mkutano na waandishi wa habari tarehe 16 Machi, 2025 katika Bandari Kavu ya Kwala, mkoani Pwani.
Amebainisha kuwa Mfumo huo pamoja na mambo mengine utakuwa na uwezo wa kusajili, kuhakiki na kuhifadhi taarifa za waandishi wa habari wote nchini
“Mwandishi wa habari atakuwa na uwezo wa kujaza taarifa na kuweka mambo muhimu kama vile picha, mahali anapofanya kazi, taarifa za uraia wake n.k, na Mfumo utatoa alama za usalama ambazo mtu hawezi kughushi,” amesema Msigwa na kuongeza;

“Kupitia mfumo huu Mwandishi wa Habari atakua na uwezo wa kuomba na kupata kitambulisho chake (physical ID). Mfumo una uwezo wa kuonesha taarifa kwenye ukurasa wa nyuma back-end ambazo zitahakikiwa na kutumiwa na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari-JAB kutoa kitambulisho (Press Card) kwa njia ya mtandao”.
Amesisitiza kuwa Mfumo utakuwa na uwezo wa kumpatia mwandishi wa habari taarifa kabla ya muda wa kuisha matumizi ya kitambulisho chake (alert when the ID is about to expire) pia utamtumia ujumbe mfupi kupitia simu ya mkononi
Msigwa amesema kupitia mfumo huo Mwandishi anapoomba kitambulisho atapatiwa namba ya malipo “control Number” ya kulipia mtandaoni na akishalipia malipo yake yataonekana na kupitishwa na mamlaka husika (approved) na kwamba utakuwa na mwonekano wa aina mbili (madirisha) kwa ajili ya waandishi wa ndani na wa nje (International)

“Mfumo utamwezesha Mwandishi wa Habari kupakia nyaraka muhimu kama vile vyeti vya taaluma kwa ajili ya uhakiki (VERIFICATION) na pia mfumo utapokea maombi ya waandishi wa nje ya nchi na wao kama ilivyo kwa wale wa ndani utawataka kupakia (Requirements) wakiwa wamekidhi vigezo ndipo hatua nyingine itafuata,” amesema.
Mfumo utakuwa na uwezo wa kuhakiki taarifa za waandishi kwa kuunganishwa na mifumo mingine ya serikali kama GePG, NIDA, NECTA, Uhamiaji n.k kwa ajili ya malipo, uhakiki wa vyeti na taarifa (Verification).
Aidha, Msigwa amesema mfumo utakuwa na uwezo wa kuondoa wale wote waliokosa sifa/wasiohuisha taarifa zao pale wanapotakiwa kufanya hivyo, utamwezesha mtumiaji kuweka saini mahali panapohusika (Digital signature) pamoja na kuruhusu taarifa za kitaaluma na eneo la kazi kupatikana kwa njia ya msimbo papo (QR CODE).
“Huduma hii ya kupata vitambulisho vya kidigitali itapatikana kwa Waandishi wa habari wote watakaokuwa wamekidhi vigezo vya kitaaluma (Taaluma ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma),”
More Stories
Kongani ya Viwanda ya Sino _Tan kutoa ajira laki moja
Waandishi wa habari kutambulika kidijitali
Mahundi awataka wanachuo kutoendekeza anasa