Na
Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema kuwa maono ya Rais Dkt. Samia ni kuhakikisha vijana wa Kitanzania wanapomaliza shule wanakuwa na maarifa na ujuzi wa kutosha wanapomaliza masomo yao kwa ajili ya maisha yao na maendeleo ya taifa.
Msigwa amesema hayo jijini hapa leo,Januari 29,2025 wakati akizungumza ba waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya uzinduzi wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2024,Toleo la 2023 ambapo inatarajiwa kuzinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. Samia Suluhu Hassan,jijini Dodoma Januari 31,2025.
Amesema kuwa lengo la Rais ni kuwaandaa wanafunzi kuwa mahiri katika kukabiliana na changamoto za sasa na kuendana na mahitaji ya dunia ya sasa.
“Mheshimiwa Rais hakupendezwa na hali ya kuwa na wahitimu wa madaraja ya juu wasio na ujuzi wa uzalishaji, hali ambayo huwasababishia changamoto za ajira na maisha pindi wanapomaliza masomo yao” amesema Msigwa.
“Kutokana na maono hayo, Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo kwa serikali kuhakikisha elimu inalenga kuwajengea wanafunzi maarifa, mwelekeo chanya, maadili na ujuzi unaokidhi mahitaji ya kitaifa na kimataifa, ili waweze kushindana katika soko la ajira duniani,”amesema Msigwa.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amesema kuwa maandalizi ya Sera pamoja na mkakati wa utekelezaji wake yamekamilika.
“Kama mnavyofahamu, Sera inatoa mwongozo wa uendeshaji na utolewaji wa elimu nchini. Mbali na Sera, tumeandaa pia mkakati wa utekelezaji, ambao utawezesha kufanikisha malengo yake,” amesema Prof. Nombo.
Ameeleza kuwa Sera hiyo imeelekeza kuboresha mitaala ya elimu kuanzia ngazi ya awali, shule za msingi kuanzia darasa la kwanza hadi la sita,Sekondari, mafunzo ya ualimu na vyuo vikuu, ili kuhakikisha elimu inayotolewa inawapa wahitimu ujuzi unaohitajika katika soko la ajira na maisha kwa ujumla.
Uzinduzi wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023 unatarajiwa kuwa hatua muhimu katika mageuzi ya elimu nchini, ukilenga kuleta mabadiliko chanya kwa kizazi cha sasa na kijacho.
More Stories
Bungua mweusi anayeshambulia zao la kahawa aibuka Bukoba
DED mpya Mbeya DC ataka watumishi kuwatumikia wananchi
Rais Samia kuzindua Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2024 Toleo la 2023