January 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Msigwa aagiza ukamilishwaji wa haraka nyaraka muhimu za uanzishwaji wa bodi ya Ithibati ya waandishi wa habari

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amemuagiza Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari Wakili Patrick Kipangula, kuhakikisha nyaraka zote muhimu zinazohitajika kwa ajili ya uanzishwaji rasmi wa Bodi hiyo zinakamilishwa mapema ili iweze kuanza kufanya kazi yake.

Msigwa ametoa agizo hilo leo wakati alipozitembelea ofisi za Bodi hiyo leo tarehe 23 Januari, 2024, Mtaa wa Jamhuri Posta, Jijini Dar es Salaam ili kufahamiana na watumishi wa Bodi, kukagua ofisi na kujionea maendeleo ya uandaaji wa nyaraka hizo kabla uzinduzi rasmi haujafanyika.

“Kwanza mimi niwapongeze sana kwa hatua mliyofikia, lakini Kaimu Mkurugenzi hakikisha unasimamia hizi nyaraka zote mlizozitaja zifanyiwe kazi kwa haraka sana na kukamilika, umuhimu wa kuanza kazi kwa bodi hii unaujua na bahati nzuri wewe ni mtu wa Sheria, ulishiriki tangu mchakato wa uandaaji wa Sheria na kanuni zake, hivyo unayafahamu majukumu yake na unafahamu kwa nini tunahitaji Bodi ya Ithibati,” amesema Msigwa na kusisitiza;

“Serikali ya Awamu ya Sita tunaona umuhimu wa kuwepo kwa hii Bodi, hivyo ni muhimu sana haya yote yaliyopangwa kufanyika yafanyike na yalete tija na manufaa kwa Tasnia ya Habari, ni muhimu sana.

Msigwa amesema baadhi ya nyaraka zinazotakiwa kufanyiwa kazi haraka ni pamoja na Muundo Bodi, Mpango Mkakati wa Bodi wa Miaka Miwili (Strategic Plan), Mkakati wa Mawasiliano wa Bodi (Communication Strategy) na Kanuni za Maadili ya Waandishi wa Habari.

Amesisitiza kuwa Mpango Mkakati wa Bodi ndiyo nyaraka na mwongozo muhimu unaoelezea malengo ya Bodi, majukumu yake, umuhimu wake, vyanzo vya mapato na namna gani taasisi itaendeshwa.

Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari ilitangazwa Septemba 18 ,2024 baada ya aliyekuwa Waziri wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Jerry Silaa kuteua Mwenyekiti wa Bodi Tido Mhando na wajumbe wake sita pamoja na sekretarieti yenye watumishi 6.

Msigwa amekuwa kiongozi mkubwa wa kwanza kuitembelea Bodi hiyo tangu ilipohamishiwa chini ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo baada ya mabadiliko ya Wizara yaliyofanywa na Rais , Dkt. Samia Suluhu Hassan, mwishoni mwa mwaka jana.