Na Penina Malundo,Timesmajira
SHIRIKA la Msichana Initiative kwa kushirikiana na shirika la Pastoral Women Council (PWC) wamewaungana na wasichana vinara 50,kutoka mikoa mitano nchini kujadili Kampeni ya pedi bila malipo huku wakiendelea kuiomba Serikali kuiondoa kodi hiyo au kufanya pedi hizo kuwa bei nafuu ili kila msichana aweze kumudu.
Mashirika hayo yameungana kwa pamoja baada ya kuona kuna changamoto kubwa wa wasichana katika matumizi ya pedi ambapo baadhi yao kutumia vifaa ambavyo sio salama kwao.
Akizungumza hayo jana jijini Dar es Salaam,Afisa Mradi kitengo cha Uchechemuzi,Wakili Lucy Gidanis amesema wasichana hao wametoka katika mkoa wa Dar es Salaam,Pwani,Tabora,Arusha na Dodoma kwa lengo la kuhakikisha wanabeba kampeni ya pedi bila kodi na watoto kupata Pedi hizo kwa bei nafuu.
Amesema tafiti zilizofanyika Mwaka 2021 na Taasisi ya NIMR pamoja na Serikali ilionesha kuwa asilimia 60 ya watoto wakike wanapata changamoto ya kupata bidhaa za kujihifadhi(Pedi) kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo hali ya uchumi kwa baadhi yao.
”Kupitia utafiti huo kama wadau tumeunganisha nguvu za pamoja kuhakikisha watoto hawa wanaweza kufanya kampeni hii ili kupata unafuu wa bidhaa hizo.

”Kupitia Mradi huu tumeweza kuwafundisha na kufanya mafunzo na wasichana vinara 50 ambao wamebeba kampeni hii katika mikoa yao mitano,hivyo leo wataonesha uwezo wao wa namna walivyobeba kampeni hiyo katika mikoa yao,”amesema Gidanis
Amesema mwaka 2018 Serikali iliporudisha kodi za Pedi,imekuwa changamoto kwa watoto kushindwa kwenda shule kwa sababu ya pedi hizo kwa sababu ya gharama kubwa hivyo wengine kupelekea kutumia vifaa ambavyo sio salama.
”Kati ya mikoa mitano tumeweza kufanikiwa kutoa mafunzo kwa watoto 10 na wao watoto wameweza kuwafikia wengine na wamejaliwa kuzungumza katika sehemu mbalimbali.
”Sisi kama wadau tunatamani sana kodi itolewe kwenye pedi ukiangalia kwenye utafiti pedi ni changamoto kubwa kwa wasichana hasa wale wenye kipato cha chini ambapo wenzetu wa nchi nyingine wamefanikiwa kutoa pedi bure,”amesema.

Amesisitiza kuwa serikali inauwezo wa kutoa kodi kwenye pedi na kugawa bure kwa watoto waliopo mashuleni au kwabei nafuu kwa watoto walio nje ya shule hii itasaidia kuwawezesha wasichana hao kuwa na amani wanapokuwa katika siku zao za hedhi.
Kwa Upande wake Afisa Mradi wa Taasisi ya PWC, Neng’ambo Thomas amesema suala la pedi bado ni changamoto katika jamii za kifugaji na kuleta gumzo kwani bado uhitaji wa elimu ni mkubwa kutokana na kutotambua kuwa kumpatia mtoto wa kike au mwanamke pedi ni sehemu ya kifaa muhimu.
”Tunaiendeleza kampeni hii kuishawishi na kuelimisha zaidi juu ya njia salama na vifaa salama ya kutumia wakati wa hedhi.
”Uelewa bado mdogo hasa kwa wanaume,ambapo ametolea mfano kwa kabila la kimasai wanakuwa na mipaka mtoto wa kike kuna sehemu unaweza kumfikia kumuelezea vitu mbalimbali ila sio suala la hedhi,”amesema.

Mmoja wa wasichana ambao ni vinara wa kampeni hiyo,Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Emanyata iliyopo Arusha,Elizabeth Mollel amesema kuwa kutokana na baadhi ya wasichana kushindwa kumudu gharama za kupata taulo za kike kila mwezi, huishia kutumia vifaa kama vile, vipande vya nguo, majani ya miti, na vifaa vingine ambavyo si salama kwa afya ya wasichana.
Amesema pakiti moja ya taulo za kike inauzwa kwa Sh2000 na inaweza kuwa juu zaidi kulingana na kampuni na mahali na msichana atahitaji kuanzia pakti mbili na zaidi ili kukamilisha mzunguko wake wa hedhi wa mwezi mmoja.
“Ukiangalia gharama hii ni kubwa sana, hasa kwa wasichana wanaotoka katika kaya masikini ambazo taulo za kike sio kipaumbele katika bajeti ya familia”
“Ukosefu wa taulo za kike unachangia wasichana kujiingiza katika tabia hatarishi na kujiingiza katika mahusiano katika umri mdogo ili apate fedha zitakazomuwezesha kununua taulo hizo.”amesema.

Aidha amesema wadau wa haki za wasichana waendelee kutoa elimu kuhusu masuala ya hedhi salama na umuhimu wa elimu ili kuendelea kubadilisha maisha ya wasichana na jamii ya kitanzania kwa ujumla.
More Stories
Mo Dewji na Urithi anaoujenga ,unavyoenda mbali zaidi ya mafanikio binafsi
Mulika Community kusaidia Serikali kukomesha vitendo vya ukatili
TMDA yashinda tuzo za PRST ya Umahiri katika kampeni bora ya utoaji elimu jamii