Na Penina Malundo,Timesmajira
HALI ya utoaji wa huduma za afya nchini zinaendelea kuboreka kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na miaka ya nyuma kutokana na mikakati pamoja na ushirikiano uliopo kati ya Serikali na wadau wa maendeleo katika kuhakikisha huduma za kiafya zinapatikana kwa ubora sahihi.
Licha ya kuwepo kwa changamoto kadhaa bado zinajitokeza katika utoaji wa huduma za afya nchini lakini kwa kiasi kikubwa hali hiyo inaonekana kupungua kutokana na ushirikiano kati ya wadau hao pamoja na serikali kuhakikisha miundombinu ya afya inakuwa salama wakati wote.
Nchi imekuwa ikishuhudia maboresho mengi yanaendelea kufanyika katika sekta hiyo ikiwemo katika uboreshwaji wa miundombinu,vifaa tiba,Dawa pamoja na kuongeza rasilimali watu kwenye sekta ya afya.
Shirika lisilo la kiserekali la Kimataifa Médecins Sans Frontières(MSF)ikimaanisha Madaktari wasio na Mipaka limekuwa miongoni mwa mashirika na wadau muhimu nchini Tanzania katika kusaidia sekta ya afya katika kuboresha miundombinu yake.
MSF iliingia nchini Tanzania mwaka1993 kutokana na mahitaji na dharura mbalimbali ikiwa ni pamoja na utoaji wa huduma za maji,afya na huduma za dharura kama kukabiliana na maradhi ya mlipuko,mahitaji ya afya ya wakimbizi na mipango mingine ya afya ili kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wahitaji.
Nchini Tanzania,Shirika linatoa huduma za afya katika kambi za wakimbizi na jamii inayozunguka kambi hizo za wakimbizi ambapo ufanya kazi kwa kushirikiana na wadau wengine na kusaidia Wizara ya afya kufanya tathmini huru ili kuamua mahitaji ya watu.
Mkurugenzi wa MSF nchini Tanzania,Tommaso Santo,anasema MSF shirika hilo ni huru la binadamu linalotoa misaada kwa watu walioathirika na vita vya silaha,magonjwa ya mlipuko na majanga ya asili.
Anasema shirika hilo limekuwa linatoa huduma za afya katika nchi zaidi ya 70.”Tunatoa msaada wa matibabu na huduma za kibinadamu zinazohitajika zaidi na kutibu kila mtu bila kujali rangi,jinsia,dini au itikadi za kisiasa.
”Mbali na huduma hizo pia wanafanya kazi kuongeza ufahamu juu ya matatizo kupitia ushahidi,kwa moyo huo walizindua kampeni ”MSF Access to Essential Medicines Campaign mwaka 1999 ili kushinikiza upatikanaji wa dawa muhimu,vipimovya uchunguzi na chanjo kwa wagonjwa katika miradi yao,”anasema.
Santo anasema walifadhili mpango huo kwa fedha za tuzo ya Tuzo ya Amani ya Nobel”Nobel Peace Prize”ambayo MSF ilizawadiwa 1999 kwa kutambua kazi inayofanywa na shirika katika maabara kadhaa na kuthamini kazi iliyofanywa na wafanyaka wao kwa kutibu mamilioni ya watu duniani kote.
Kwa upande wake Mratibu Msaidizi wa Huduma za Afya kutoka Shirika la Madaktari Wasiokuwa na Mipaka(MSF),Florian Mwebesa,anasema tangu mwaka 2015 Shirika liliingia Tanzania likisaidia wakimbizi waliotoka Burundi mkoani Kigoma wilayani Kibondo katika kambi ya Nguta.
Anasema shirika lilianza kutoa huduma ya afya kwa wakimbizi na kwa jamii inayozunguka katika kambi hiyo na kutoa huduma ya afya ya dharura na huduma ya afya ngazi ya pili.
”Huduma hii inahusiana na wagonjwa wa magonjwa ya dharura ,mama akitaka kujifungua na kulazwa pamoja na Mama wenye uhitaji wa upasuaji hivyo tunashirikiana na Wizara ya Afya kuwapeleka katika Hospitali ya rufaa ya Kibondo na kufanyiwa upasuaji.
”MSF pia imekuwa ikitoa misaada ya kisaikolojia pamoja na matibabu ya ukatili wa kijinsia katika kambi hiyo ambayo watu wanakumbana nazo,”anasema.
Aidha Mwabesa anasema mbali na mradi huo,mwingine MSF inayofanya ni pamoja na mradi wa Liwale ambao ulisaidia mradi wa Mama na Mtoto ambao ulianza mwaka 2022,ulipanga kuhakikisha wanapunguza vifo vya wamama na watoto.
Anasema kwa kipindi hicho wilaya hiyo ya Liwale vifo ya wamama wajawazito vilikuwa zaidi ya asilimia nne na tangu wameanza kufanya kazi wameshusha hadi chini ya asilimia moja huku kwa upande wa watoto waliochini ya umri wa miaka mitano vifo vyao vilikuwa zaidi ya asilimia 23 hadi 25 lakini MSF imeshuka hadi asilimia saba hadi 15.
”Tupo katika mafanikio makubwa na mazuri kwani wakati tulikuwa tunaenda liwale huduma za upasuaji ilikuwa zaidi 25 lakini tumeweza kushusha kwa sasa hadi kufikia Asilimia 10 kwa namna tunavyofanya kazi kwa kushirikiana na Serikali,”anasema .
Akizungumzia mradi wa Magonjwa ya Mlipuko kwa Tanzania,Mwabesa anasema mwaka 2023 mwezi machi kulitokea mlipuko wa Murbugy ambapo MSF imesapoti kuwapa mafunzo watoa huduma kuona namna gani wanaweze kuwatibu wagonjwa na kutoa huduma kwa watu ambao wameathirika na ugonjwa huo.
Anasema MSF imeweza kupiga hatua ya kuiwezesha Serikali katika shughuli mbalimbali ikiwemo ya kuondoa taka katika vituo vya afya vinavyotoa huduma kwa waathirika wa magonjwa ya mlipuko,kutoa vifaa vya kuzuia watu kujikinga na watoa huduma za afya kujikinga na ugonjwa huo.
Anasema wamekuwa wakifanya kazi kwa karibu na watoa huduma za afya ngazi ya jamii ni ujumbe gani wanatakiwa kuufikisha kwa jamii ili watu kujizuia na ugonjwa huo.
”Katika ugonjwa wa mlipuko wa Kipindupindu,MSF imekuwa inafanya kazi kwa ukaribu na Wizara ya afya Kitengo cha Magonjwa ya Mlipuko mwaka huu tulianza na eneo la Nanjilinji Wilayani Kilwa ambapo kulikuwa na ugonjwa huo wa mlipuko ambapo tulisaidia kwa kiasi kikubwa na sasa tupo Nzinga ambapo tunatoa huduma za matibabu kwa wagonjwa ambao wamekumbwa na ugonjwa huo.
”Pia tumekuwa tunatoa msaada wa kutoa elimu kupitia watoa huduma wa elimu ya afya ngazi ya jamii ambao wanatoa elimu namna ya kujizuia ,kuosha mikono,kutumia vyoo na kula chakula cha moto kufunikia vyakula ili kujikinga na ugonjwa huo,”anasema.
Mbali na mradi huo pia MSF imekuwa ikitoa dawa za kutibu maji kwasababu wanajua ugonjwa wa kipindupindu ambao unaambukiza kwa kupitia maji na chakula chenye vimelea vya kipindupindu ambapo wamesaidia kutoa elimu ya kujadiliana kwa kupitia watoa huduma wa ngazi ya jamii.
”Kwa sasa pia tupo simiyu ambapo kuna mradi tunaisaidia Serikali katika ugonjwa wa mlipuko,wilayani Itilima ambapo tunafanya kazi kama tulivyofanya Kilwa kusaidia jamii kujikinga na ugonjwa wa kipindupindu,”anasema.
More Stories
NIDA yawakumbusha wananchi kuchukua vitambulisho vyao
Dkt.Kafumu:Uteuzi wa Rais Samia umezingatia katiba
Kliniki ya sheria bila malipo yazinduliwa Kilimanjaro