Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
BOHARI ya Dawa (MSD) imesema usambazaji wa dawa na vifaa vya kisasa Kisiwani Mafia mkoani Pwani umefanikiwa kupunguza rufaa za wagonjwa kutoka kisiwani humo kwenda kutibiwa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza leo kisiwani Mafia Afisa Huduma kwa Wataeja wa MSD wa kanda hiyo Diana Kimario, alisema bohari hiyo imefanikiwa kupunguza rufaa za wagonjwa kutoka kisiwani Mafia kwenda jijini Dar es Salaam kwa kufunga vifaa tiba vya kisasa hususani vya maabara na upasuaji.
“Wilaya hii ina vituo vya afya 25 ambapo vituo 21 vipo Mafia na vituo vine vipo katika visiswa vidogo, ambapo vifaa vilivyosambazwa na MSD vitafanikisha kupunguza changamoto ya rufaa kwa wagonjwa waliokuwa wakisafirishwa kwenda jijini Dar es Salaam kwa ajili ya huduma,”alisema.
Amesisitiza kuwa wamefanikiwa kusambaza Xray mashine, vitandaa vya kuchangia damu, mashine za kusaidia upumuaji, jenereta kubwa na ndogo na vifaa vingine vyenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 450,”alisema.
Diana amesema hatua hiyo imefikiwa kutokana na maboresho makubwa yaliyofanywa na Rais Dk.Samia kwa hospitali hiyo kuwa na majengo ya kisasa yanayokidhi vifaa vilivyofungwa hususani jengo la dharula na wagonjwa mahututi (ICU).
Amesema, pamoja na mafanikio hayo wamekuwa wakikutana na changamoto ya usafirishaji wa dawa na vifaa tiba kutokana na tozo wanazokutana nazo bandarini hivyo wanaiomba serikali kuona namna ya taasisi husika ikiwemo wilaya, MSD na bandari kukaa pamoja na kutoa msamaha kwa bidhaa za afya.
“Kuleta gari ya dawa na vifaa tiba Mafia ni gharama unalipia kivuko na kodi kwa bandari na Nyamisati na Mafia na iwapo tutashindwa kulipia inatulazimu kushusha mzigo na kupakia katika meli na wanapofika Mafia kutafuta gari ndogo za serikali au za kukodi kusambaza ambapo usambazaji unachukua muda mwingi.”
“Kutokana na hali hiyo MSD Kanda ya Dar es Salaam tumeomba kukutana na wenzetu uongozi wa wilaya, Mbunge, uongozi wa kivuko na bandari waone namna ya kusamehe kodi katika bidhaa za afya,”amesema
Naye Mganga Mkuu wa Wilaya Dk. Maulid Majala amesema hospitali hiyo imepokea zaidi ya sh.milioni 550 kwa ajili ya ujenzi wa majengo mapya mawili na sh.bilioni 1.39 kwa ajili ya vifaa tiba hivyo anatoa wito kwa watumishi kuhakikisha uwekezaji huo unaendana na thamani ya huduma zinazotolewa.
Amesema ujenzi wa majengo hayo na vifaa vya kisasa ni muhimu, kwa kuwa awali walikuwa wakikutana na wagonjwa wa dharula hususani wa ajali inawaladhimu kuwapa rufaa kutokana na hospitali hiyo kukosa vitendea kazi.
Dk.Majla ameeleza ujio wa bidhaa hizo za afya na upatikanaji wa dawa kutoka asilimia 60 hadi 90 umeboresha utoaji wa huduma kisiwani Mafia.
Naye Mganga Mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Mafia ambaye ni daktari bingwa wa wanawake Dk.Said Maya, amesema kutokana na mazingira ya kisiwa hicho wanaishukuru MSD kwa kazi kubwa inayoifanya kuhakikisha dawa na vifaa tiba vinafika hadi vituoni bila kujali changamoto za mazingira yaliyopo.
More Stories
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato
Wambura asikitishwa na makundi CCM Nyakato