Na Daudi Manongi,TimesMajira Online. Dodoma
NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Mary Maganga amemwelekeza Msajili wa Hazina kutochambua bajeti yoyote, itakayowasilishwa nje ya mfumo wa kielektroniki wa Planrep.
Mary ameyasema hayo leo wakati akifungua mafunzo ya Matumizi ya Mfumo Mpya wa Uandaaji na Uwasilishaji wa Bajeti na Taarifa za Bajeti ki-elektroniki wa PlanRep katika Wakala za Serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma jijini Dodoma.
“Ili kuwezesha ufanisi katika usimamizi wa mali za umma, ilihitajika pamoja na mambo mengine kuwa na mifumo madhubuti ya kielektroniki itakayorahisisha usimamizi wa rasilimali hizo,” amesema.
Amesema hadi kufika Juni mwaka 2019, serikali ilikuwa imewekeza katika taasisi, mashirika ya umma na kampuni zinazomilikiwa na serikali kwa hisa chache 266, zenye uwekezaji wa kiasi cha sh. trilioni 59.6 na kudhihirisha uhitaji wa mifumo ya kielektroniki.
Akieleza faida za mfumo huo Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka amesema uwepo wa mfumo huo utasaidia kuimarisha usimamizi wa matumizi ya fedha za umma katika mashirika na taasisi za umma, pamoja na upatikanaji wa taarifa za uhakika na kwa wakati.
Pia kupunguza gharama kubwa za fedha za umma katika ununuzi, uundaji, usimikaji, uendeshaji na usimamizi wa mifumo hiyo pamoja kupunguza utitiri wa mifumo ya kibajeti ya kieletroniki iliyoanzishwa bila kupata ridhaa ya Wizara ya Fedha na Mipango, ambayo ni Msimamizi Mkuu wa fedha na mali za umma.
More Stories
Mhagama atoa somo kwa watendaji
Ilemela nyama choma festival, yazinduliwa
Mchengerwa:Rufaa 5,589 za wagombea zimekubaliwa