November 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mradi wa ujana salama wanufaisha vijana 815 Kakonko

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Kakonko

SERIKALI ya awamu ya 6 kupitia mradi wa ujana salama ambao ni sehemu ya mpango wa kunusuru kaya maskini nchini (TASAF), imetoa zaidi ya sh mil 142.7 katika kipindi cha mwaka 2022 na 2023 kwa ajili ya kuwezesha kiuchumi vijana 815 Wilayani Kakonko Mkoani Kigoma.

Hayo yamebainishwa hivi karibuni na Mratibu wa TASAF Wilayani humo, Eusebia Michael Barantanda alipokuwa akiongea na vyombo vya habari vilivyotembelea wilaya hiyo ili kujionea mafanikio ya mradi huo.

Alisema kati ya mwezi Mei na Agosti wilaya ilipokea ruzuku ya biashara kiasi cha sh mil 87.5 na kuzigawa kwa vijana 515 wenye umri kati ya miaka 14-19 wanaotoka katika familia za walengwa wa TASAF waliotambuliwa katika vijiji 32.

Kutokana na kiasi hicho kila kijana alipata mgao wa sh170,000 kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi wa kiuchumi aliobuni ili kumuingizia kipato.

Eusebia aliongeza kuwa Machi 31, 2023 halmashauri ilipokea kiasi kingine cha sh mil 59.1na kukigawa kwa vijana wengine 300 kutoka katika kaya za walengwa waliotambuliwa kutoka vijiji 12 vilivyobakia na kila kijana akapata sh 184,000 ili kuanza kutekeleza biashara aliyobuni.  

‘Tunaishukuru sana serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha mpango wa TASAF na kuanzisha mradi wa ujana salama, mradi huu ni mkombozi kwa vijana walio wengi, ni ajira tosha inayowaingiza kipato’, alisema.

Alifafanua kuwa kabla ya kupewa fedha hizo walipewa elimu ya stadi za maisha na afya ya uzazi ili kuhakikisha wanaingia kwenye utu uzima wakiwa na ufahamu wa kutosha wa elimu ya stadi za maisha na afya njema ya kuendesha maisha yao.

Alibainibisha kuwa hadi sasa vijiji vyote 44 vilivyoko katika wilaya hiyo vimenufaika na mradi huo na vijana 348 waliopo katika vijiji 12 vilivyoingizwa katika mpango wa TASAF mwaka jana wamepewa mafunzo hayo.  

Baadhi ya vijana walionufaika na mradi huo Martha Lukindo mkazi wa kijiji cha Itumbiko na Joseph Lulamye mkazi wa kijiji cha Muganza katika kata ya Kakonko waliishukuru serikali kwa kuwapatia mitaji ili kuanzishia miradi yao ya kiuchumi.

Naye Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo Emanuel Mhene alisema mradi wa ujana salama ni sehemu ya utekelezaji ilani ya uchaguzi ya chama ili kuinua vijana kiuchumi, hivyo akampongeza Rais Samia kwa ubunifu mkubwa na kusimamia kwa dhati utekelezaji ilani ya uchaguzi.

Aidha alipongeza halmashauri ya wilaya hiyo kwa kutambua kaya maskini za watu wenye ulemavu zipatazo 1,528 na kuziingiza katika mpango wa TASAF wa kuhawilisha kaya maskini na sasa zina uhakika wa kupata milo 3 kwa siku.