January 19, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mradi wa maji wa miji 28 kunufaisha wakazi 3700 kaliua

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

MRADI wa maji unaotekelezwa na serikali ya awamu ya sita katika Miji 28 nchini kwa gharama ya sh bil 143.26 unatarajiwa kunufaisha wakazi zaidi ya 3,700 katika halmashauri ya Wilaya ya Kaliua Mkoani hapa.

Akiweka jiwe la msingi katika moja ya miradi hiyo jana Wilayani humo, Waziri wa Maji Juma Aweso alisema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025.

Alisema ilani hiyo inabainisha wazi kuwa ifikapo mwaka 2025 upatikanaji huduma ya maji safi na salama ya bomba katika maeneo ya mijini itakuwa imefikia asilimia 95 na vijijini itafikia asilimia 85.

Waziri Aweso alibainisha kuwa hali ya upatikanaji huduma ya maji katika wilaya hiyo bado siyo wa kuridhisha, kwani mahitaji halisi kwa wakazi wa wilaya hiyo ni wastani wa lita mil 16.9 kwa siku.

Na kuongeza kuwa kwa sasa wilaya hiyo inapata maji chini ya wastani huo ambayo ni lita mil 7.9 kwa siku hivyo kufanya Wilaya hiyo kuwa na upungufu wa lita mil 8.9 kwa siku.

Waziri alibainisha kuwa mahitaji kwa wakazi wa Mji wa Kaliua pekee kwa siku ni lita mil 1.5 wakati uzalishaji ni lita laki 6.75 hivyo kupelekea upungufu wa lita laki 8.6 na kufanya hali ya upatikanaji huduma ya maji safi na salama katika mji huo kuwa asilimia 44 tu.

Kwa upande wa vijijini Aweso alisema mahitaji ni lita mil 15.42 kwa siku ila kiasi kinachozalishwa ni lita mil 7.25 tu hivyo kuwa na upungufu wa lita mil 8.17 na kufanya hali ya upatikanaji maji vijijini kufikia asilimia 49Alibainisha kuwa mradi wa Miji 28 katika Mkoa huo utatekelezwa katika wilaya 3 za Kaliua, Urambo na Sikonge kwa gharama ya sh bil 143.26 na maji yake ni yale ya kutoka Ziwa Victoria ambayo kwa sasa yamefika mjini Tabora.

Mradi huo unatekelezwa na kampuni ya Megha Infrastructure Company Limited ya nchini India na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwaka 2025.

Aliwataka wataaluma wa Mamlaka ya Usambazaji Maji Tabora (TUWASA) wanaosimamia mradi huo kuhakikisha unakamilika kwa wakati ili wananchi waweze kunufaika hivyo kumaliza kilio chao cha muda mrefu.

Awali Mkurungezi Mtendaji wa Mamlaka hiyo Mhandisi Mayunga Kashilimu alimweleza Waziri Aweso kuwa kukamilika kwa mradi huo uliogharimu kiasi cha shil mil 503 kutanufaisha wakazi wapatao 3700.

Katibu Tawala wa Mkoa huo (RAS) Dkt John Mboya alimwomba Waziri aelekeze Mamlaka hiyo (TUWASA) kujenga Ofisi katika Mji wa Kaliua na ihusike kusambaza maji katika eneo lote la Mji huo na Wakala wa Usambazaji Maji Vijijini (RUWASA) ahusike tu kusambaza maji vijijini wazo ambalo lilikubaliwa na Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo.