September 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mradi wa maji wa bil.4.21 chanzo afya bora kwa wananchi Mpimbwe



Na George Mwigulu,Timesmajiraonline, Mpimbwe.

MRADI wa maji safi na salama wa thamani ya Bil 4.21 utasaidia kuokoa maisha ya wananchi ambao kwa wakati tofauti wameripotiwa baadhi kupoteza maisha hususani watoto wadogo kwa sababu ya kuugua magonjwa ya mlipuko.

Wananchi wa halmashauri ya Mpimbwe Mkoa wa Katavi wameonekana kufurahishwa na kuzinduliwa kwa mradi huo na kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa 2024, Godfrey Mnzava leo September 9, 2024 katika kata ya Mbede.

Kwani mradi huo umejibu sehemu ya ripoti ya mpango jumuishi wa taifa wa malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto 2021/22 hadi 2025/26 unaotaka uwekezaji unaoratibiwa kwenye maeneo matano  ya mfumo wa malezi jumuishi ambayo ni Afya bora, Lishe, Malezi, Ulizi na Usalama.

Mkazi wa kijiji cha Nyambwe, Sophia Tungu amesema “ Mwanangu alipoteza maisha kwa ugonjwa wa kuhara niliambiwa na watalamu wa afya kuwa inanipasa kuchemsha maji ili yawe safi na salama kuepuka magonjwa”.

Sophia ameeleza kuwa kukosekana kwa afya bora na kifo kulisababishwa hapo awali kwa kukosa huduma ya maji salama ambapo anaamini maji safi ni sehemu ya kukamilisha lishe bora kwa familia yake.

“Namshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa sasa kama mnavyoona maji mazuri tunapata bila shida yoyote na ninafuraha kubwa sisi kwetu watu wa vijijini kuona mradi unaziduliwa”amesema Sophia.

Shija Ng’wanzalima, Mkazi wa kijiji cha Minyoso amesema mradi wa maji kutoka Majimoto hadi Usevya utawaondolea kero wanawake wengi ambao kwa kiasi kikubwa ni watendaji wa majukumu yote ya nyumbani.

Amesema wanawake muda mwingi hutumia kutafuta maji ambapo kwa wakati mwingine hapo awali walilazimika kutembea umbali mrefu zaidi kwenda kuchota maji na pindi wanaporudi kwa kuchelewa majumbani hufanyiwa vitendo vya kikatili hasa kupigwa na waume zao kwa wivu wa mapenzi.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024, Godfrey Mnzava akizindua mradi huo amesema kuwa licha ya maji hayo kuwahudumia wananchi lakini maeneo yote ya taasisi yapate hati miliki ili kuondoa migogoro kuweza kujitokeza kwenye miradi mikubwa kama hiyo ya maji.

“Na kama mwananchi mwenyewe atakuwa ameamua kutoa kwa ajili ya maslahi ya umma na  baada ya taasisi  kupewa  kinachofuata ni kupata hati miliki ambapo lazima utaratibu ufikie mwisho na sio kukwama katikati” Amesema.

Mnzava wakati akizindua mradi huo alitoa muda wa wiki mbili kuhakikisha mchakato wa eneo hilo la mradi unakamilika kwa haraka kwa ajili ya kuweka mazingira mazuri ya mradi huo kuendelea kuhudumia wananchi bila kujitokeza mgogoro wowote.

Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mlele, Mhandisi Charles Mengo wakati akisoma utekelezaji wa mradi huo wa maji safi na salama alieleza kuwa mradi huo unahudumia vijiji vya Usevya, Msadya, Nyambwe, Ikuba na Minyoso kwa fedha za mpango wa lipa kwa matokeo kwa mkataba wa miaka mitano.

Amefafanua kuwa upanuzi wa mradi huo unatumia chanzo cha maji Mamba chenye uwezo wa kuzalisha maji lita 180 kwa sekunde ambapo kabla ya utekelezaji wa mradi huo, huduma ya maji ilikuwa inapatikana kupitia visima  virefu na visima vya pampu za mkono.

Mhandisi, Mengo ameogeza kuwa mradi huo ulikusudiwa kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama katika vijiji vitano kutoka skimu ya Majimoto na wakazi 34,650 watanufaika na mradi huo.