January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mradi wa Joroadhi Ngozi Kuanza na Megawati 30 za Umeme

Na Penina Malundo,Timesmajira

KAMPUNI ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) imesema tayari mradi wa uzalishaji umeme wa megawati 70 unaotokana na jotoardhi katika eneo la ziwa Ngozi wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya upo katika hatua ya uhakiki wa rasilimali na kisha uchorongaji ili kuanza uzalishaji kwa kuanza na Megawati 30 za umeme.


Hayo yalibainishwa jana na Mjiokemia Mwandamizi kutoka TGDC, Ariph Kimani wakati akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (sabasaba) yanayoendelea kwenye viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.

Kimani amesema watashirikiana kwa pamoja na Wizara ya Nishati katika kuhakikisha wanazalisha umeme wa Jotoardhi haraka iwezekanavyo huku wakiendelea kutoa elimu ya Jotoardhi kwa wadau mbalimbali.
Alisema lengo la kutoa elimu hiyo kwa wadau ni kuhakikisha watanzania wanakuwa na uelewa mpana zaidi kuhusu mradi huo wa kimkakati ambao unatekelezwa na Taasisi yao.
Kimani amesema Kampuni yao ina miradi mitano ya kipaumbele ambayo ni Ngozi unaotajiwa kuzalisha Megawati 70 lakini kwa kuanzia wataanza na Megawati 30, Mradi wa Kiejo- Mbaka utakaozalisha Megawati 60 yote hii ikiwa mkoani Mbeya, Mradi wa Songwe mkoani Songwe utakaozalisha Megawati 5 hadi 38, Mradi wa Luhoi mkoani Pwani utakaozalisha Megawati 5 na Mradi wa Natroni mkoani Arusha utakaozalisha Megawati 60.

Amesema mpaka sasa miradi yote hiyo iko katika hatua mbalimbali ambapo nguvu kubwa imeelekezwa katika Mradi wa Ngozi na wakati wowote uchorongaji kwa lengo la uhakiki unatarajia kuanza.


”kwa sasa tunaendelea kukamilisha hatua mbalimbali za manunuzi ili kuchoronga visima vya Jotoardhi lengo likiwa ni kuhakiki rasilimali iliyopo chini ili ituwezeshe kwenda hatua itakayofata ya kuchoronga visima vikubwa Zaidi kwa ajili ya uzalishaji. Hivyobasi, pindi taratibu hizo zitakapokamilika tutashuhudia hatua hii muhimu katiaka utafutaji wa nishati hii adhimu na jadidifu ya jotoardhi, ”amesema


Ameongeza kuwa, baada ya kukamilisha mradi huo wataweza kuendelea na miradi mingine waliyoifanyia utafiti kama mradi wa Songwe uliopo Kijiji cha Nanyala wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, kisha mradi wa Kiejo-Mbaka uliopo Halmashauri Wilaya Busokelo wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, Luhoi Wilayani Rufiji Mkoa wa Pwani na mradi wa Natron Mkoani Arusha.


“Mpaka sasa Tanzania tuna viashiria vya jotoardhi takribani 52 katika mikoa 16 ambapo tayari tumeviainisha na tunaendelea na tafiti za awali na kwamba kati ya vyote, ni maeneo manne yapo katika hatua ya uhakiki,”amesema.