Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Korogwe
VIONGOZI wa Vijiji kwenye kata za Vugiri na Lewa katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga wamesema Mradi wa Forests, Rights and Livelihoods (FORLIVES) umeweza kuwasaidia kurudisha uoto wa asili kwenye misitu ya asili kwa wananchi wa vijiji vinne baada ya kupewa elimu huku wakiwezeshwa ili kutunza mazingira.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi leo Machi 27,2025 kwa nyakati tofauti mara baada ya hafla fupi ya utiaji saini wa Mipango ya Usimamizi wa Misitu na Sheria Ndogo za Vijiji vya Mashindei, Vugiri, Bagamoyo na Old Ambangulu iliyofanyika Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, Makuyuni walisema wamepata faida kupitia mradi huo
Bakari Kilindikuu, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji Mashindei, Kata ya Lewa amesema
wanatunza mazingira kwa kushirikiana na Shirika la TFCG, ambapo wanafanya mikutano ya hadhara na kukubaliana kama kijiji na kuweka Sheria Ndogo, kuwa mtu akiingia ndani ya msitu anachukuliwa hatua. Na ulinzi huo umefanikiwa baada ya kuchagua Kamati za Mazingira za Vijiji ambazo zinaundwa na watu 10, hivyo kila kitongoji wanatoka watu wawili.

“Kamati ya Mazingirara kazi yao kubwa ni kupanga mipango ya mazingira ambapo wanapanga kama ni kwenda kwenye kuni kwa wiki mara mbili, Jumatano na Jumamosi. Hivyo mtu atakaekwenda kinyume na hapo, amekiuka maagizo. Na adhabu yake ni faini ndogo ndogo kuanzia sh. 20,000 hadi 50,000″amesema Kilindikuu.
Naye Rajab Gao ambaye ni Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mashindei amesema changamoto ni nyingi kulinda misitu, lakini sasa wananchi wameanza kuelewa baada ya kupata elimu juu ya kutunza mazingira eneo la Kijiji cha Mashindei ambacho kina hekta 1,025 za misitu.
Na kwa elimu waliyopata kutoka Mradi wa FORLIVES, wameweza kulinda vyanzo vya maji, kupanda miti kwenye vyanzo vya maji, na kuweza kufanya doria mara mbili kwa wiki kupitia Kamati ya Mazingira ili kuzuia uhalifu wa vyanzo vya maji na misitu.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Old Ambangulu, kilichopo Kata ya Vugiri, Rogers Elia alisema wamewahamasisha wananchi kulima kilimo cha kutunza mazingira. Kuna wataalamu wanakwenda kutoa elimu ya kulima kwa kuchimba matuta, matumizi ya mbolea ya asili ya samadi na mboji.

Kaimu Ofisa Mtendaji Kijiji cha Old Ambangulu, Elifuraha Felisian amesema moja ya kazi zinazofanywa na jamii mara baada kupewa elimu, ni upandaji wa miti kwenye vyanzo vya maji, na kufuga mifugo kisasa kwa kufungia ndani mifugo hiyo ikiwemo kutolisha mifugo kwa kuzurura.
“Mradi wa FORLIVES umesaidia kutokukata miti ovyo, suala la kuondoa ufugaji kwenye misitu, kilimo ndani ya misitu, ambapo zamani watu walikuwa wanalima ndani ya msitu, lakini sasa hawafanyi hivyo”amesema Felisian.
Naye Julius Mntambo ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Vugiri amesema mradi huo umeweza kutoa elimu kwa wananchi juu ya uhifadhi wa mazingira, kuwezesha kuanzisha vikundi na kuviwezesha pembejeo mbalimbali ikiwemo mbegu, mbolea, na wataalamu kuanzisha vitalu vya miche ya miti kama mikarafuu, pilipili manga, mdalasini kwa ajili ya shughuli za kiuchumi na utunzaji wa mazingira.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Vugiri Bituni Kopwe alisema zile changamoto zilizowekupo za wananchi kuvamia misitu na kuvuna miti zimeondoka baada ya wananchi kupata uelewa. Shirika la TFCG wamekuwa wakitenga siku mbili kwa wiki kwa ajili ya wananchi kuchukua kuni ndani ya hifadhi za misitu, na hiyo imesaidia kuzuia watu kuingia msituni mara kwa mara.
Akizungumza kwenye hafla hiyo Meneja wa Mradi wa FORLIVES Bettie Luwuge alisema ni mradi mmoja wapo unaotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG). Mradi una dhumuni la kuimarisha na kuwawezesha jamii zinazotegemea misitu kwa kusimamia haki zao za ardhi na maliasili kupitia usimamizi endelevu wa misitu na ardhi, na kuboresha maisha ya jamii katika Kata ya Lewa, na Vugiri, kwenye vijiji vya Mashindei, Vugiri, Bagamoyo na Old Ambangulu.

Luwuge amesema vijiji hivyo vipo eneo lenye umuhimu wa Bioanuwai la Tao la Mashariki (West Usambara). Mradi unapata ufadhili wa miaka mitatu (2023- 2025) kutoka Shirika la Danmission kutoka nchi ya Denmark. Shirika la Danmission ni la kidini na linadhamiria kuona dunia ambayo watu wanaishi pamoja kwa amani katika mazingira yao.
“Mradi una matokeo makuu matatu, Mosi; Jamii zinazoishi kandokando mwa hifadhi za misitu katika Milima ya Usambara Magharibi zinanufaika moja kwa moja na matumizi endelevu ya rasilimali za misitu ifikapo mwishoni wa mwaka 2025. Pili: Jamii zinazoishi pembezoni mwa Milima ya Usambara Magharibi zimeboresha mbinu za kilimo kufikia mwaka 2025, na tatu; Uwezo wa jamii zinazoishi pembezoni mwa Milima ya Usambara Magharibi na taasisi za kidini umeimarika katika nyanja mbalimbali zinazopelekea utumiaji endelevu, utekelezaji thabiti na usimamizi bora wa maliasili kufikia mwaka 2026″amesema Luwuge.
Luwuge amesema utambulisho wa mradi wa FORLIVES katika ngazi za vitongoji hadi vijiji ulitambulishwa kwa wananchi kwenye vijiji vyote vinne kuanzia ngazi za vitongoji (25) na kwenye mikutano ya wajumbe wa Serikali za vijiji na mikutano mikuu ya vijiji vyote mwishoni mwa Februari 2024. Uhamasishaji kuhusu dhana ya ushirikishwaji na Usimamizi wa Misitu ya Vijiji (USM) pamoja na kupendekeza wajumbe wa Kamati za Maliasili za vijiji. Mikutano hii ya uhamasishaji katika ngazi za vitongoji pia ilifanya kupata uwakilishi wa wajumbe wawili kila kitongoji kuwa sehemu ya Kamati ya Maliasili ya Kijiji zenye wajumbe 10 hadi 12 kila Kijiji wakizingatia jinsia.
“Kutoa mafunzo na kuwajengea uwezo wanajamii kwa Kamati za Maliasili na Wajumbe wa Serikali za vijiji kuhusu majukumu yao kwenye nyanja za utawala bora, sera na sheria, jinsia, uongozi,, doria, uwekaji wa kumbukumbu za fedha. Wanajamii zaidi ya 200 walipewa mafunzo kwa kushirikiana na wataalamu wa halmashauri”amesema Luwuge
Akifungua hafla hiyo ya utiaji saini
Mipango ya Usimamizi wa Misitu na Sheria Ndogo za Vijiji, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Sadick Kallaghe, aliwataka viongozi wa vijiji wakishirikiana na wananchi kuendelea kuhifadhi misitu kwa vizazi vya sasa na vile vijavyo kwa ajili ya kupata maji, na kupata hewa safi.


More Stories
EWURA kinara uhusiano mwema na vyombo vya habari nchini
TANESCO yaibuka kinara tuzo za ubora za Mawasiliano na Uhusiano kwa umma 2024
Taasisi za uhifadhi zatakiwa kulinda maeneo ya hifadhi kwa teknolojia