Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Kaliua
SERIKALI imesikia kilio cha wakazi wa Vijiji vya Wachawaseme na Kazana-upate katika kata ya Igagala, Wilayani Kaliua Mkoani Tabora baada ya kukamilisha ujenzi wa zahanati itakayohudumia wakazi 30,000 wa vijiji hivyo.
Akizindua zahanati hiyo jana Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka huu Abdallah Shaib Kaim alipongeza jitihada kubwa zinazoendelea kufanywa na serikali ya awamu ya sita kwa kuboresha huduma za kijamii.
Alibainisha kuwa ujenzi wa zahanati hiyo ya kisasa ni mkombozi kwa wakazi wa vijiji hivyo kwa kuwa sasa wataweza kupata matibabu karibu na nyumbani kwao tofauti na huko nyuma ambapo walilazimika kutembea umbali mrefu.
‘Nawapongeza kwa usimamizi mzuri wa mradi huu, thamani ya fedha imeonekana kwa kile kilichofanyika, ila hakikisheni mnautunza vizuri ili jamii inufaike zaidi’, alisema.
Alisisitiza kuwa ujenzi wa mradi huo na miradi mingine yenye thamani ya sh bil 2.3 iliyokaguliwa, kuwekewa mawe ya msingi na kuzinduliwa na mwenge huo wilayani humo ni sehemu ya juhudi kubwa zinazofanywa na Mheshimiwa Rais.
Awali akisoma taarifa ya mradi huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Dkt Amin Vasomana alisema mradi huo ambao umegharimu zaidi ya sh mil 179 utahudumia wakazi 22,737 wa Kijiji cha Wachawaseme na 7,378 wa Kijiji cha Kazanaupate.
Alibainisha kuwa mradi huo umemaliza kilio cha muda mrefu kwa akinamama wajawazito, watoto na wazee ambao walikuwa hawawezi kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya katika vijiji jirani.
Dkt Vasomana alieleza kuwa baada ya kuanza kutoa huduma jumla ya akinamama wajawazito 8 wamejifungua salama katika kituo hicho ndani ya wiki moja tu na kuongeza kuwa hakuna mama mjamzito atakaye poteza maisha tena.
Aidha aliongeza kuwa wateja 123 wamepata huduma za kliniki ya baba, mama na mtoto na wateja 137 wamepatiwa huduma za wagonjwa wa nje (OPD) na kubainisha kuwa wakazi wa vijiji hivyo sasa wanafurahia kusogezewa huduma za afya karibu.
Mbunge wa Jimbo la Kaliua Aloyce Kwezi alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea fedha za kujengwa zahanati hiyo, adha ya kutembela umbali mrefu sasa basi.
Alibainisha kuwa ujenzi wa zahanati hiyo, nyumba ya watumishi na miradi mingine ya mabilioni ya fedha inayoendelea kutekelezwa na Rais katika wilaya hiyo ni sehemu ya utekelezaji ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
More Stories
Watoto wenye uhitaji wapatiwa vifaa vya shule
Wananchi Kisondela waishukuru serikali ujenzi shule ya ufundi ya Amali
RC.Makongoro ataka miradi itekelezwe kwa viwango