Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Njombe
WIZARA ya Mifugo na Uvuvi inaandaa mpango wa unywaji maziwa katika shule zote nchini ili kuhakikisha ifikapo mwaka 2025 kila shule ya msingi inakuwa na programu za kunywa maziwa.
Hayo yamesemwa jana na Katibu Mkuu (Mifugo) Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Elisante Ole Gabriel wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Njombe.
Amesema Wizara yake inaandaa mapendekezo yatakayoshirikisha Wizara ya Elimu, Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa pamoja na wadau mbalimabli ili kuweza kutekeleza Mpango wa huo wa unywaji maziwa katika shule zote hapa nchini.
“Lengo ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2025, kila shule ya msingi iwe na programu za kunywa maziwa shuleni na kila Mtanzania awe anakunywa angalau lita 100 kwa mwaka,” amesisitiza.
Amesema kufanyika kwa maadhimisho hayo mkoani Njombe imekuwa ni chachu ya kuwashawishi wadau wa maziwa, viongozi wa Serikali, wa kisiasa na dini kushirikiana na wazazi na washiriki wengine wa maendeleo kuhakikisha Mpango huo unatekelezwa katika shule zote nchini.
Amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi imejipanga vizuri kuhakikisha uzalishaji wa maziwa unaongezeka ikiwa ni pamoja na kuongeza ushirikiano na wadau wa tasnia ya maziwa nchini.
Prof. Ole Gabriel amesema hadi kufikia Septemba, 2020 shule 210 zenye wanafunzi 89,922 zimenufaika na mradi wa maziwa shuleni katika mikoa 10 ya Kilimanjaro, Arusha, Tanga, Dar es Salaam, Iringa, Mbeya, Njombe, Morogoro, Mwanza na Mara ambapo Jumla ya lita 12,023,186.83 za maziwa zenye thamani ya takribani sh. bilioni 19.24 zimenywewa katika vipindi tofauti kuanzia mwaka 2006 hadi 2020.
Amesema kwa mwaka 2020/2021 programu za unywaji maziwa zinaendelea kutekelezwa katika shule 30 nchini kutoka shule 210 zilizokuwa zikitekeleza mapango huo hapo awali.
Mikoa inayotekeleza mpango huo kwa sasa na shule zake kwenye mabano ni Kilimanjaro (Shule 24), Iringa (Shule 2) na Mbeya (Shule 4) kwa ushirikiano wa Wazazi na wasindikaji.
Ametoa mwito kwa Watanzania wote kujenga utamaduni wa kunywa maziwa yaliyosindikwa na bidhaa zake pamoja na kula nyama bora zilizozalishwa, kuchakatwa na kukaguliwa na wataalamu wa mifugo nchini.
“Aidha, tujizoeze sisi na watoto wetu kutumia bidhaa za mazao ya mifugo zilizosindikwa na kuchakatwa ikiwa pamoja na maziwa freshi, mgando, jibini, samli, siagi, ice cream na hata maziwa ya unga.
Bidhaa zote hizi ni bora, salama, zinajenga afya bora na kuongeza kiwango cha ufahamu kwa watoto,” amesisitiza Profesa Ole Gabriel
*** Sekta ya uvuvi
Kwa upande wa Sekta ya Uvuvi, amesema inachangia asilimia ya protini inayopatikana na inatoa ajira kwa Watanzania takribani milioni 4.5 katika shughuli mbalimbali zinazohusiana na Sekta ya Uvuvi.
Amefafanua kuwa katika mwaka 2019/20, Sekta ya Uvuvi ilikua kwa kiwango cha asilimia 1.5 na kuchangia Pato la Taifa (GDP) kwa asilimia 1.71. Uzalishaji wa samaki kutoka maji ya asili kwa mwaka 2019/20 umefikia takribani tani 392,933.0 na katika uzalishaji wa mazao ya viumbe maji kufikia tani 18,716.56.
Vile vile, amesema kumekuwepo na ongezeko la uwingi (biomass) wa samaki katika maji yetu hususan katika Ziwa Victoria ambapo samaki aina ya Sangara wameongezeka kutoka tani 417,936 mwaka 2016 hadi tani 816,964 mwaka 2020, sawa na ongezeko la asilimia 95.5. Aidha, uzalishaji/uvunaji wa samaki katika maji ya asili umeongezeka kutoka tani 362,645 mwaka 2015/2016 hadi tani 497,567 mwaka 2019/2020.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa