November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mpango: Mama atasema jambo hivi karibuni

Ni kuhusu nyongeza ya mishahara, asema ni endapo hali ya sasa itadumu, watumishi 81,515 wapandishwa hadi kufikia 2023/24

Na Penina Malundo, Timesmajiraonline, Arusha

RAIS Samia Suluhu Hassan, amewahakikishia wafanyakazi kwamba endapo hali ya sasa itadumu, wawe na matumaini kwamba atasema jambo hivi karibuni.

Kauli hiyo ilitolewa na Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango, ambaye alimwakilisha Rais Samia kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Mei Mosi yaliyofanyika mkoani Arusha, jana.

Dkt. Mpango amesema kama ambavyo wamekuwa wakisema, Serikali itaendelea kuhuisha viwango vya mshahara kwa kuzingatia uwezo wa kiuchumi na kibajeti pamoja na ujuzi na utendaji wa waajiriwa.

Amesema misingi hii ni muhimu ili kuepuka kuchochea mfumuko wa bei, kuhatarisha uhimilivu wa deni la Taifa na athari nyingine kwenye utulivu wa uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akitoa zawadi ya ujumla kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambao wameongoza katika michezo mbalimbali katika kuadhimisha ya Siku ya Wafanyakazi Duniani ambayo Kitaifa imefanyika katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Mkoani Arusha tarehe 01 Mei 2024.

“Haya yote lazima yazingatiwe katika mchakato wa kuongeza mishahara, hususan katika kipindi hiki ambapo uchumi wa dunia umekumbwa na misukosuko mingi ikiwemo vita baina ya Urusi na Ukraine, vita ya Mashariki ya Kati inayohusisha Israel, Palestina, Lebanon, Syria, Iran na Yemen.

Vita hivyo vimepelekea kuvurugika kwa mfumo wa ugavi na kupanda sana kwa bei za mafuta, mbolea, chuma na chakula,” alisema Dkt. Mpango na kuongeza.

“Kama hiyo haitoshi, dunia imekumbwa na majanga mengine ikiwemo mvua kubwa na maporomoko ya ardhi ambayo yamesababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu, magonjwa na hata vifo.”

Amesema changamoto zote hizi zimeathiri uchumi wetu. Hata hivyo, alisema pamoja na changamoto hizi, tathmini ya Serikali na ya Taasisi za kimataifa ikiwemo IMF, Benki ya Dunia, AfDB, Moody’s, Fitch n.k. zimeonesha kuwa uchumi wa Taifa umekuwa stahimilivu kwa kiasi cha kuridhisha.

“Nchi yetu inakopesheka na ina mvuto kwa wawekezaji wa moja kwa moja kutoka nje, hivyo, Mama ameniagiza niwaambie wafanyakazi wa Tanzania kuwa endapo hali hii itadumu, wawe na matumaini kwamba atasema jambo hivi karibuni,” amesema.

Aidha, amesema pamoja na hatua hiyo, Serikali imeendelea kuboresha maslahi ya watumishi kwa namna nyingine mbalimbali, ikiwemo kwa kulipa nyongeza ya mwaka ya mshahara (annual salary increment), ambapo Mwaka 2023/24 kiasi cha sh. 153,926,496,703.68 kililipwa; na kwa mwaka 2024/25, Serikali imetenga sh. 150,873,245,100.00 kwa ajili hiyo.

Viongozi mbalimbali wa Serikali na Sekta Binafsi wakiwa kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani ambayo Kitaifa imefanyika katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Mkoani Arusha tarehe 01 Mei 2024.

“Kama mlivyosema kwenye risala yenu, kabla ya mwaka jana, nyongeza ya mshahara ilikuwa imesimama kwa muda mrefu, lakini sasa tunajitahidi kuitekeleza.

Kwa upande mwingine, Serikali imeendelea kuwapandisha vyeo watumishi mbalimbali, ambapo Mwaka 2023/24 jumla ya watumishi 81,515 walipandishwa vyeo na mwaka 2024/25 Serikali imetenga kiasi cha 252,703,717,483.72 kwa ajili ya kuwapandisha vyeo watumishi 219,924,” amesema Dkt. Mpango.

Amewapongeza wafanyakazi wote nchini kwa kuadhimisha sikukuu hii, na nawashukuru tena kwa mchango wenu adhimu katika ujenzi wa Taifa letu. Kama yalivyo makundi mengine kwenye jamii, kundi la wafanyakazi lina mchango mkubwa sana katika ujenzi wa nchi yetu. Serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya kazi ikiwemo kuboresha maslahi ya wafanyakazi kadri hali ya uchumi itakavyoruhusu.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia Viongozi na Wafanyakazi kutoka Wizara, Taasisi za Serikali na Binafsi wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani ambayo Kitaifa yamefanyika katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Mkoani Arusha tarehe 01 Mei 2024.

“Wito wangu kwenu wafanyakazi, ni kuendelea kutekeleza majukumu yenu kwa bidii, maarifa, uadilifu na kwa moyo wote, huku mkitanguliza maslahi ya Taifa mbele.

Nawaomba pia muendelee kuongeza tija katika utendaji kazi. Navisihi vyama vya wafanyakazi tushirikiane na Serikali na Waajiri kuhakikisha tunaongeza tija kwenye maeneo yetu ya kazi kwa manufaa ya Taifa na wafanyakazi wenyewe, sambamba na kupaza sauti kuhusu madai ya wafanyakazi,” amesema Rais Samia.

………