January 18, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Moto wateketeza samani za mamilioni Tabora

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

MOTO mkubwa umezuka jana katika Mtaa wa Toronto katika halmashauri ya manispaa Tabora na kuteketeza maduka 3 yaliyokuwa yamejaa mali za wafanyabiashara zenye thamani ya mamilioni ya fedha.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoani hapa  Mohamedi Shomari alisema moto huo umetokea jana majira ya 4.10 asubuhi.

Alisema Timu ya Zimamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama (Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi) walifika eneo la tukio  mara tu baada ya kupata taarifa kutoka kwa wananchi na kuanza kuzima moto huo.

Alisema juhudi za kuudhibiti moto huo zilifanikiwa kuokoa baadhi ya mali za mamilioni ya fedha zilizokuwa katika maduka hayo na stoo ya kuhifadhia mali.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani hapa ACP Richard Abwao alisema mmiliki wa duka mojawapo aliyeunguliwa duka lake alidondoka na kupoteza fahamu baada ya kukuta duka lake likiteketea ambapo alikimbizwa hospitalini.

Alisema Jeshi hilo kwa kushirikiana na Shirika la Umeme (TANESCO) wanaendelea na uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha moto huo .

Alisema baada ya kukamilika kwa uchunguzi huo watatoa taarifa kwa umma hivyo akataka wafanyabiashara hao kuwa watulivu. 

Shuhuda wa tukio hilo ambaye ni mfanyabiashara aliyekuwa jirani na eneo hilo, Matata Saidi Matata alisema mmoja wa wafanyabiashara Juma White aligundua moto huo baada ya kufungua duka lake na kukuta moto ndani ila ulikuwa bado  haujashika kasi ambapo alianza kupiga kelele kuomba msaada.

Alisema alitoka nje haraka na kuomba msaada wa wenzake huku akichukua bodaboda na kwenda kutoa taarifa Ofisi za Jeshi la Zima Moto na Uokoaji.

Alibainisha kuwa licha ya Vikosi vya Uokoaji kufika eneo la tukio na kusaidia kuzima moto huo, vilikuwa havitoshi, hivyo akaomba serikali kuwaongezea magari ya  Zima Moto ili kuepusha uharibifu mkubwa wa mali za wananchi.