Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online. Songea
KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Kamishna Msaidizi wa Polisi, Simon Maigwa amewataka maofisa na askari wa Jeshi la Uhifadhi wa Wanyamapori kujiepusha na vitendo vya rushwa kwa kutoruhusu wafugaji kuingiza mifugo katika mapori na hifadhi za taifa.
Ameyasema hayo mjini hapa jana wakati wa hafla kuwavisha vyeo maofisa kumi na askari watano wa kikosi dhidi ya ujangili na wa pori la akiba Liparamba, iliyofanyika katika ofisi za Kikosi cha Kuzuia Ujangili Kanda ya Kusini Songea.
Amewataka maofisa na askari hao kutumia weledi, moyo wa kujituma na kutanguliza uzalendo katika kupambana na wahalifu mbalimbali, wakiwemo majangili ambao wanaingia kwenye hifadhi na kuuwa wanyama, ambao ni urithi na rasilimali kubwa za taifa.
“Nawaomba sana maofisa na askari msijihusishe na vitendo vya rushwa kuruhusu wafugaji na majangili kuingia katika hifadhi zetu, nendeni mkapambane bila kuchoka ili kuhakikisha hifadhi zetu zinabaki salama kwa ajili ya maslahi ya taifa,” amesema Kamanda Maigwa.
Pia amewataka watumishi hao kuendelea kuwatumikia Watanzania kwa uadilifu na uaminifu, ili kujenga taifa na kutokata tamaa katika majukumu yao ya kila siku.
Amesema moja ya sifa ya askari ni uvumilifu kwa hiyo ni lazima askari, atambue pindi adui anapovamia pori anatahitajika kwenda mstari wa mbele kupambana bila kuchoka kwa kuwa wapo baadhi ya maadui, waliopitia mafunzo ya jeshi na wengine hata kupata mafunzo ya ugaidi.
More Stories
Maofisa Watendaji watakiwa kufanya kazi kwa weledi
Muhoji Sekondari kumaliza changamoto ya umbali kwa wanafunzi Musoma vijijini
Tanzania mwenyeji mkutano wa nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika