December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mo Dewji achomoza bilionea pekee Afrika Mashariki

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Dar

MAZINGIRA mazuri ya uwekezaji nchini yamezidi kuleta matunda baada ya Jarida la Forbes kumtaja mfanyabiashara, Mohammed Dewji maarufu Mo, kuwa bilionea pekee kutoka Afrika Mashariki, aliyeingia katika orodha ya mabilionea 18 Afrika.

Dewji, pia ametajwa na Forbes kushika nafasi ya 13 kati ya 18 ya mabilionea wa Afrika na namba moja Afrika Mashariki na Kati, akiwa na utajiri wa dola za Kimarekani bilioni 1.5.

Mo ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya MeTL Group, amepanda kutoka kuwa bilionea namba 15 Afrika kwa mwaka 2022 hadi bilionea wa 13, huku akitoa nafasi za ajira 35,000 kutoka 28,000 katika biashara zake.

Tangu kuingia madarakani mwaka 2021, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amekuwa akiweka mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi; hatua ambayo imemnufaisha bilionea Mo Dewji, ambaye ameongeza utajiri na nafasi yake miongoni mwa mabilionea wa Afrika.

Pia, mazingira hayo mazuri ya biashara yaliyowekwa na serikali ya Rais Samia yamemfanya Mo Dewji kuongeza nafasi hizo za ajira ambazo zinawanufaisha vijana na watu wa rika tofauti, ambao wengi ni Watanzania.

Mo Dewji anaongoza kampuni ya MeTL inayomiliki viwanda vinavyozalisha bidhaa mbalimbali zikiwemo za vyakula, kutoa huduma za usafiri na pia kupitia Mfuko wa Mo Dewji Foundation amekuwa akishirikiana na serikali kutoa msaada na ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu wenye mahitaji maalumu, katika fani mbalimbali ikiwemo ya udaktari.

Pia, kupitia Mpango wa Kuboresha mazingira ya Biashara nchini (Blueprint), serikali imerahisha mazingira ya upatikana wa vibali vya kazi, uwekezaji na huduma nyingine zikiwemo za Mamlaka ya Mapato kuwa katika sehemu moja (One stop center).

Vinara wengine

Pia, jarida hilo limeendelea kumtaja bilionea Aliko Dangote raia wa Nigeria, amabye ni mwekezaji nchini Tanzania, kuwa bilionea namba 1 Afrika kwa miaka 12 mfululizo, akiwa na utajili wa dola za Marekani bilioni 13.5.

Bilionea namba mbili Afrika ni Johann Rupert raia wa Afrika Kusini, akiwa na utajiri wa dola za Marekani bilioni 10.7, bilionea namba tatu ni Nicky Oppenheime raia wa Afrika Kusini, mwenye utajiri wa dola za marekani bilioni 8.4, bilionea namba nne ni Abdulsamad Rabiu, raia wa Nigeria akiwa na utajii wa dola za marekani bilioni 7.6.

Wengine ni Nassef Sawiris, raia wa Misri anashika nafasi ya tano, akiwa na utajiri wa dola za Marekani bilioni 7.3, Mike Adenuga raia wa Nigeria anashika nafasi ya sita, akiwa na utajiri wa dola za marekani bilioni 6.3, Issad Rebrab raia wa Algeria anashika nafasi ya saba akiwa na utajiri wa dola za Marekani bilioni 4.6, Naguib Sawiris raia wa Misri anashika nafasi ya nane akiwa na utajiri wa dola za Marekani bilioni 3.3.

Nafasi ya tisa inashikiliwa na Patrice Motsepe, raia wa Afrika Kusini akiwa na utajiri wa dola za Marekani bilioni 3.2, nafasi ya kumi ni Mohammed Mansour raia wa Misri, akiwa na utajiri wa dola za Marekani 2.9, raia Misri, nafasi ya 11 ni Koos Bekker, raia wa Afrika Kusini akiwa na utajiri wa dola za Marekani 2.6, nafasi ya 12 ni Strive Masiyiwa, raia wa Zimbabwe akiwa na utajiri wa dola za Marekani bilioni 1.9.

Nafasi ya 13 ni Mohammed Dewj raia wa Tanzania, akiwa na utajiri wa dola za marekani bilioni 1.5 akifungana na Aziz Akhannouch, raia wa Morocco na Youssef Mansour, raia wa Misri wote wakiwa na utajiri wa dola za Marekani bilioni 1.5, nafasi ya 16 ni Othman Benjelloun raia wa Morocco, akiwa na utajiri wa dola za Marekani bilioni 1.3, 17 ni Michiel Le Roux raia wa Afrika Kusini, akiwa na utajiri wa dola za Marekani bilioni 1.2 na 18 ni Yasseen Mansour, raia wa Misri akiwa na utajiri wa dola za Marekani bilioni 1.1, akifungana na Christoffel Wiese raia wa Afrika Kusini.