October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

MNEC ataka jumuiya za Chama kuwa na uchumi imara

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora        

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Mohamed Nassoro Hamdan (Meddy) amesema atahakikisha chama hicho kinaendelea kuwa imara zaidi na kuwezesha jumuiya zake kuwa na uchumi wa uhakika.

Akiongea na gazeti hili Ofisini kwake jana alisema CCM ni chama kilichobeba matumaini ya Watanzania hivyo katika kipindi chake cha miaka 5 atahakikisha kinakuwa imara zaidi na kufufua miradi ya kiuchumi kwa kila jumuiya.

Alibainisha kuwa hana shaka na nguvu ya chama hicho katika Mkoa huo, kwa kuwa kina watendaji wazuri katika ngazi zote na wanasiasa waliobobea, ila kinahitaji usimamizi thabiti ili kuwa imara zaidi kiuchumi na kisiasa.

Alisisitiza kuwa atahakikisha jumuiya zote (Vijana, Wanawake na Wazazi) zinakuwa na miradi yenye tija, itakayowaingizia kipato ili kufanikisha utekelezaji majukumu yao ya kila siku ikiwemo kuunganisha wanachama wao.

Aliongeza kuwa amepanga kutembelea wilaya zote 7 za Mkoa huo na kukutana na Viongozi na Watendaji wa Chama na Jumuiya zake ili kuhamasisha uhai wa chama na kushirikishana fursa za kiuchumi zilizopo katika maeneo yao.

Meddy alifafanua kuwa huu ni wakati kujenga chama ili kiendelee kuwa na nguvu zaidi kwa kuwaunganisha wanaCCM wote kuwa kitu kimoja, aliwataka kuweka makundi yao ya uchaguzi pembeni ili kujenga chama imara zaidi.

 ‘Uchaguzi umeisha, naomba wanaCCM wote tuwe kitu kimoja, tujenge chama chetu, tudumishe umoja na mshikamano wetu, tofauti zetu za uchaguzi zisitugawe ili kufanya vizuri zaidi katika uchaguzi ujao wa serikali za mitaa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu wa 2025’, alisema.

Alisisitiza kuwa mafanikio makubwa ambayo chama kimepata tangu kuanzishwa Februari 5, 1977 yametokana na umoja na mshikamano wa viongozi na wanachama, hivyo kudumisha mafanikio hayo hawana budi kuwa kitu kimoja.

Aidha alisema Chama na Jumuiya zake zikiwa na uchumi imara zitaweza kufanikisha utekelezaji majukumu yao ikiwemo kutembelea wanachama na wananchi kwa ujumla, kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi.

Meddy alimpongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia ipasavyo utekelezaji ilani ya uchaguzi ya chama ikiwemo kujenga chama imara.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Mohamed Nassoro Hamdan (Meddy) wa nne kutoka kulia akiwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora, Hassan Waksuvi ( aliyevaa kofia) na Viongozi wengine wakiwa katika moja ya shughuli za kujenga chama na Jumuiya zake Wilayani Urambo Mkoani Tabora hivi karibuni. Picha na Allan Vicent.