Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
HOSPITALI ya Muhimbili tawi la Mloganzila, imewataka watanzania wenye shida ya magoti na nyonga wajitokeze kwaajili ya kambi ya upasuaji kutoka kwa wataalamu wa ndani watakaoshirikiana na wabobezi kutoka nchini India.
Kambi hiyo ya itakayoanza tarehe 26 mwezi huu hadi tarehe 30 itafanyika kwenye hospitali ya Mloganzila ambapo mamia ya watu wenye matatizo ya aina hiyo watafanyiwa upasuaji.
Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Upasuaji wa hospitali ya Mloganzila, Goodlove Mfuko, alisema watakaojitokeza watafanyiwa uchunguzi wa kina na kisha watafanyiwa upasuaji kwenye kambi hiyo ambayo ni ya pili kufanywa na hospitali hiyo.
Alisema jana kuwa maandalizi yote yamekamilika na kwamba kwenye kambi hiyo watashirikiana na mtaalamu kutoka hospitali kubwa nchini India ya Yashoda, Dk. Ram Mohan Reddy.
“Mtaalamu huyu atashirikiana na madaktari bingwa ambao ni wataalamu wa mifupa na ajali hapa Mloganzila, hii itakuwa mara ya pili kutoa huduma kama hii kwani mara ya kwanza tuliwafanyia upasuaji wa kubadilisha nyonga na magoti wagonjwa 170 kwa mafanikio makubwa,” alisema
“Kwa hiyo kwenye kambi hii ambayo ni ya pili tutashirikiana na daktari huyu mbobezi kutoka India kupata uzoefu ili tuweze kubadilishana naye uzoefu ili tuboreshe zaidi huduma zetu,” alisema
“Kwa hiyo watu wenye matatizo ya nyonga na magoti wafike Mloganzila mapema ili wafanyiwe uchunguzi wa mapema kwaajili ya kupewa hiyo huduma ya kubadilisha nyonga na magoti,” alisisitiza Dk. Mfuko.
Naye daktari bingwa wa mifupa wa Mloganzila, Dk. Joseph Amos ambaye amebobea kwenye upasuaji wa nyonga na magoti, alisema kambi hiyo itahusisha upasuaji wa magonjwa yote yanayohusisha nyonga na magoti.
“Tutakuwa na mtaalamu kutoka India ambaye ni bingwa wa upasuaji wa nyonga na magoti mwenye uzoefu wa miaka 20, atakuja na watalamu wenzake hapa Mloganzila kufanya upasuaji huu,” alisema
Alisema hospitali ya Mloganzila imeshaandaa mchakato unaoendelea kwa sasa wa kuwatambua watu wenye matatizo ya nyonga na magoti utakaoendelea mpaka tarehe 24 mwezi huu siku chache kabla ya kambi hiyo.
“Utambuzi huu unahusisha maumivu katika magito, maumivu katika nyoga watakapofika kwenye kliniki zetu watafanyiwa uchunguzi wa kina na wataalamu wetu waliobobea kwenye matibabu hayo. Tutawatambua ni wangapi watafanyiwa upasuaji na wangapi watafanyiwa matibabu ya kawaida,” alisema Dk. Amos
More Stories
Mhandisi Samamba awasisitiza maafisa madini kusimamia usalama wa migoni msimu wa mvua
Wapinzani kutimkia CCM ishara ya ushindi Uchaguzi Serikali za Mitaa
Vikundi Ileje vyakabidhiwa mikopo ya asilimia 10, DC Mgomi avipa somo