November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkuu wa Wilaya Kishapu awaangukia Sumajkt akiomba umeme, ombi lake lapokelewa

Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kampuni ya Umeme SUMAJKT, Meja James Mhame (kushoto) akiwa pamoja na mkuu wa kituo cha Shinyanga, Peter Gwandu wakitazama moja ya michoro itakayotumika katika kusambaza umeme kwenye vijiji vya wilaya ya Kishapu.

Na Suleiman Abeid, Timesmajira Online

MKUU wa wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Joseph Mkude amewaomba wakandarasi wanaosambaza umeme wa vijijini (REA) SumaJKT kuipatia umeme shule mpya ya Sekondari ya Ikonda ili kuwezesha wanafunzi kupata muda mwingi wa kujisomea.

Mkude ametoa ombi hilo mbele ya Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kampuni ya Umeme SUMAJKT ambapo amesema dhamira ya Serikali kusambaza umeme vijijini ni pamoja na kuhakikisha umeme huo unafika kwenye Taasisi zote ikiwemo shule na Zahanati.

“Shule hii ya Sekondari ni shule mpya ambayo imejengwa kwa fedha ambazo zimetolewa na Rais Samia Suluhu Hassan, hivyo nikiambiwa haitopatiwa umeme sintosikia raha, na sintolala usingizi hata Rais Samia hatopata furaha,”

“Kama amewekeza fedha nyingi kwa ajili ya kuokoa maisha ya watoto wetu kutembea umbali mrefu, madarasa manane yamekamilika, madarasa mawili yako usawa wa mtambaa panya, nyumba nne za walimu zinajengwa, mbili kwa moja kila moja, leo hii tukichengesha umeme kwenye eneo hili, hatutaeleweka,” ameeleza Mkude.

Mkuu huyo wa wilaya amewaomba SUMAJKT kuangalia uwezekano wa kuipatia umeme shule hiyo pamoja na kuisaidia kuiwekea miundombinu ya nyaya na vifaa vyake vyote vinavyohitajika ili watoto waweze kusoma vizuri na kwamba lengo la Serikali kupeleka umeme vijijini ni pamoja na maeneo yote kupata umeme huo.

Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kampuni ya SUMAJKT, Meja James Mhame amemtoa wasiwasi mkuu wa wilaya Shkwa kueleza kuwa shule hiyo iko katika mpango wa kufikishiwa umeme kama ilivyo kwa maeneo mengi ya Taasisi za kiserikali na kidini.

“Katika awamu hii shule hii imepata umeme, hapa tuliposimama pana nguzo, maana yake walimu watapata umeme na madarasa yatapata umeme, lakini kwenye hili suala la kuweka mifumo ya ndani ili madarasa, mabweni na madarasa ziweze kupatiwa mfumo halisi wa umeme nitalifikisha kwenye uongozi wa juu,” ameeleza Meja Mhame.

Majengo ya vyumba vya madarasa katika Shule ya Sekondari Ikonda, kata ya Itilima wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.
Mkuu wa wilaya ya Kishapu, Joseph Mkude na wakandarasi Kampuni ya Umeme ya SUMAJKT wakikagua ujenzi wa nyumba mbili za walimu zinazojengwa kwenye Shule ya Sekondari Ikonda kata ya Itilima iliyopo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.