December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkuu wa Mkoa azindua wiki ya sheria mkoani Tabora

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online

MKUU wa mkoa wa Tabora, Balozi Dkt.Batilda Burian amezindua wiki ya sheria katika mkoa wa Tabora, Katika hafla hiyo ambayo ilipata kuhudhuriwa na jopo la majaji likiongozwa na Jaji Amour Said Khamis, Jaji Mfawidhi Mahakama kuu kanda ya Tabora, viongozi wa serikali na wananchi waliojitokeza.

Kabla ya kufika na kutoa hotuba yake katika viwanja wa Chipukizi, Dkt. Batilda aliwaongoza wananchi katika maandamano ya amani ambapo wadau mbalimbali wa sheria waliweza kutoa elimu kupitia mabango yenye kubeba kauli mbiu isemayo “Umuhimu Wa Utatuzi Wa Migogoro Kwa Njia Ya Usuluhishi Katika Kukuza Uchumi Endelevu: Wajibu Wa Mahakama Na Wadau.”

Katika hotuba yake, Dkt. Batilda alianza kwa kutoa shukrani na pongezi kwa majaji na wadau wa mahakama ya kanda mkoani Tabora kwa kusimamia vema sheria na kuleta usawa katika jamii.

Amewataka wananchi watambue kuwa uwepo wa mahakama ni ishara ya uwepo wa utawala wa sheria kwa mujibu wa katiba ya Tanzania kwa maslahi ya Umma. Awataka majaji na wadau wa mahakama kutambua nafasi yao katika kutatua migogoro mbalimbali inayowakabiri wananchi.

Aidha kipekee Mhe Mkuu wa Mkoa ameelezea chimbuko la usuluhishi wa migogoro kwa njia ya mazungumzo toka enzi za baba wa Taifa Mwl. Nyerere ambapo alisaidia kuwepo kwa mazungumzo ya amani ya usuluhishi wa mgogoro wa Burundi.

Mkuu wa Mkoa alimwelezea Dkt.Samia Suluhu Hassan Kama kinara wa wakati huu katika usuluhishi wa migogoro kwa njia ya mazungumzo kwa kuwezesha maridhiano baina ya vyama vyetu vya siasa na kuelekeza umuhimu wa maridhiano na ujenzi wa nchi kwa pamoja kupitia 4Rs yaani Reconciliation, Resilience, Reforms and Rebuding.

Awataka watumishi wa mahakama, wadau na wananchi kutumia wiki hii ya sheria mkoani Tabora, kwa kuimarisha uwajibikaji.

Awataka wananchi na wadau kutambua taasisi na vyombo mbalimbali vinavyojihusisha na masuala ya usuluhishi wa migogoro kama vile Baraza la Habari Tanzania (MCT) Pamoja na bodi ya wakandarasi.Awashukuru mamia ya wananchi waliojitokeza kwa wingi katika uzunduzi huo.