Na Mwandishi wetu, TimesMajira
Jumuiya ya Wanataaluma wa Kiislamu Tanzania (TAMPRO) Jumapili hii, Desemba 26, 20121, inatarajiwa kufanya mkutano wake wa mwaka jijini Dar es Salaam, huku moja ya ajenda kuu ikiwa ni kupitisha mpango mkakati wa miaka minne ambao utakuwa dira ya maendeleo kwa kipindi hicho.
Mwenyekiti wa TAMPRO, Haji Mrisho amesema mpango huo wa miaka minne ukitekelezwa unatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika utendaji kazi wa jumuiya hiyo yenye jukumu la kuhudumia Waislamu na Watanzania kwa ujumla kwa kutumia taaluma za wanachama wake.
“Mpango mkakati huu unagusa na kuchora ramani ya utekelezaji miradi ya huduma zote muhimu ambazo jumuiya yetu inashughulika nazo ikiwemo elimu, afya, dini, uchumi, miundombinu, habari na tehama,” alisema Mrisho.
Kwa mujibu wa Haji Mrisho mgeni rasmi katika mkutani huo anatarajiwa kuwa Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, huku kauli mbiu ya mkutano huo ikiwa ni ‘Utaalamu na mshikamano katika kuihudumia jamii.’
Naye Katibu wa Jumuiya hiyo, Sharif Mohammed alisema kuwa maandalizi ya mkutano huo utakaofanyika katika ukumbi wa Golden Jubillee Towers yanaendelea vizuri ambapo wajumbe takriban 100 wanatarajiwa kuhudhuria, huku wengine wakishiriki kutoka mbali, ikiwemo nje ya nchi, kwa njia ya mtandao.
Mkutano mkuu huo unafanyika takriban miezi miwili tangu jumuiya hiyo yenye mchango mkubwa katika maendeleo ya Uislamu ichague viongozi wake wapya, ambapo Mrisho alichaguliwa kuwa Mwenyekiti huku Dkt Abubakar Kijoji akichaguliwa kuwa makamu wake.
TAMPRO ina wanachama kutoka kada zote za kitaaluma wakiwemo walimu, madaktari, wahandisi, wanazuoni wa kidini, wahadhiri wa vyuo. Pia, TAMPRO ina matawi katika mikoa kadhaa, ingawa katika mpango wake mpya wa miaka minne inatarajiwa kuanzisha matawi nchi nzima.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja