March 1, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO kufanya ziara siku sita nchini

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Audrey Azoulay, anatarajiwa kuwasili nchini Machi 1, 2025 kwa ziara ya siku sita.

Ziara hiyo inafuatia mwaliko wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo alimkaribisha kufanya ziara nchini.

UNESCO ni mshirika wa Tanzania kwa miaka mingi kwenye masuala ya elimu, sayansi na utamaduni.Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mwanachama wa UNESCO na ilijiunga na Shirika hili mnamo Machi 6, 1962 kwa Agizo Na. 337 la Baraza la Mawaziri (Cabinet Order) la Tanganyika na kuanzisha Tume ya Taifa ya UNESCO.

Baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Mwaka 1964, masuala ya UNESCO yalikuwa ni mambo ya Muungano na Tume ya UNESCO ikawa ni ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mwaka 2008 Tume ilitungiwa Sheria Na. 7 ya mwaka 2008 (The UNESCO National Commission Act, 2008) ambayo iliipa hadhi kuwa chombo huru cha serikali kinachojitegemea kikiwa na jukumu la kupanga, kuratibu, kuhamasisha, kusimamia, kutathmini na kutekeleza kazi zote za UNESCO katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akiwa hapa nchini, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO atafanya mazungumzo na mwenyeji wake,Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dr. Hussein Ali Mwinyi.

Pamoja na kukutana na Marais, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO atatembelea eneo lililo katika orodha ya UNESCO ya Urithi wa Dunia wa Kitamaduni la Mji Mkongwe wa Zanzibar na eneo lililo katika orodha ya UNESCO ya Binadamu na Hifadhi Hai ya Mazingira (Man and Biosphere Reserve) la Rufiji, Mafia, Kibiti na Kilwa (RUMAKI) katika kisiwa cha Mafia.

Akiwa nchini,Azoulay atatangaza mradi wa maji chini ya ardhi katika mwambamaji wa Mlima Kilimanjaro unaoandaliwa na Tanzania na Kenya kwa kushirikiana na UNESCO na utafadhiliwa na Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi (The Global Environmental Facility).

Mradi huu utabaini na kuwezesha kuchorwa ramani ya maeneo yenye maji ya kutosha ambayo kwa baadaye inaweza kutumika kuongoza maeneo ya kuchoronga na kuweka miundo mbinu ya kuwapatia wananchi maji ya uhakika katika eneo la Kilimanjaro.

Aidha, Azoulay akiwa Zanzibar, atatembelea majengo mashuhuri ikiwemo Palace Museum, Bait Al Ajaib, Majestic Cinema, Soko la Watumwa, Kanisa la Mkunazini na pia atatembelea shamba la viungo kizimbani na kuonana na vikundi vya akina mama na katika eneo hilo atapanda mche wa mkarafuu.