NA Joyce Kasiki, Timesmajira Online, Dodoma
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mkenda Profesa Adolf Mkenda amewaasa wadau wa Elimu kujadili kwa kina kuhusu elimu ya ufundi stadi kulingana na mageuzi ya elimu yajayo hatua ambayo itawawezesha vijana kutatua changamoto zilizopo katika jamii kulingana na elimu wanayoipata shuleni.
Profesa Mkenda ameyasema hayo leo Desemba 06,2022 wakati wa Mkutano wa mwaka wa Tathmini ya Maendeleo ya Sekta ya Elimu mwaka 2021/22 uliofanyika jijini Dodoma.
“Kuna mageuzi ya elimu ambayo yanakuja ,kama wadau wanapaswa kujadili suala hilo kwa kina kwa kuwa elimu yetu kwa kiasi fulani lazima iongeze ufundi stadi ili kuwawezesha wahitimu wa ngazi zote za elimu kutumia ujuzi waanaoupata darasani kujiajiri.”amesema Profesa Mkenda
Amesema sekta ya Elimu nchini bado inahitaji mageuzi makubwa hivyo anaamini kupitia mkutano huo Wadau watapata nafasi ya kujadili kikamilifu namna ya kuleta maendeleo endelevu kwenye sekta ya Elimu ambayo inahitaji kuongeza ufundi Stadi kama ilivyoelekezwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan .
“Hatua hii itawafanya vijana kuwa vijana wenye ubunifu na ujuzi wa kutosha pale wanapohitimu elimu,hivyo Mkutano huu wa Wadau utatusaidia ni namna gani ya kuingiza hicho kipengele katika Mitaala yetu,” Amesema Prof.Mkenda
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt.Francis Michael amesema kuwa kaulimbiu ya Mkutano huo wa mwaka wa Tathmini ya Maendeleo ya Sekta ya Elimu mwaka 2021/22 ni “Marekebisho ya Mifumo ya Elimu ili Kukidhi Mahitaji ya Kitaifa na Kimataifa” ,hivyo ni vyema kila mmoja aliyepata fusa ya kushiriki mkutano huu kujadili kwa kina mada zitakazowasilishwa na kutoa maoni yenye tija katika kuimarisha na kuendeleza elimu yetu nchini.
Amesema kaulimbiu hiyo inaakisi mwelekeo wa Serikali katika kuleta mageuzi katika Sekta ya Elimu kama ilivyoelekezwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba katika kutekeleza azma hiyo ya marekebisho na maboresho katika sekta, Wizara inaendelea na maboresho ya mitaala kuanzia ngazi ya Elimumsingi hadi Elimu ya juu.
“Aidha, uboreshaji wa Sera ya Elimu unaendelea baada ya ukusanyaji wa maoni ya wadau wa elimu nchini kote na kuendelea kuyachakata,”Amesisitiza
Dkt.Francis ameongeza kuwa kupitia Mikutano hiyo ya tathimini ambayo imekuwa ikifanyika kila mwaka ,yamepatikana mafanikio mbalimbali yaliyopatikana, ikiwemo Ukarabati na ujenzi wa miundombinu ikiwemo madarasa, mabweni, maabara na matundu ya vyoo kwa Shule za Msingi na Sekondari,Ukarabati wa miundombinu ya Taasisi za Elimu ikiwemo Vyuo Vikuu (SUA, ARDHI, MZUMBE, UDSM, Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Ametaja mafanikio mengine ni Kuajiri Walimu 11,547 (ambapo 7928 ni wa Shule za Msingi pamoja na walimu 3,621 wa Shule za Sekondari),Kutoa Mafunzo kwa Walimu 402 wanaotoa mafunzo kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum;
Pia Dkt.Francis amesema Kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania imeandaa miongozo ya utoaji wa elimu kwa kutumia TEHAMA kwa elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Vyuo vya Ualimu na Kukamilisha Mpango wa Maendeleo wa Sekta ya Elimu 2021/22 -2025/26.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Elimu UNESCO ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wadau wa Maendeleo katika Sekta ya Elimu Tanzania Faith Shayo amesema kuwa Mkutano huo umekuja Muda Muafaka kwani Dunia kupitia Umoja wa Mataifa ipo katika mabadiliko na mageuzi katika Sekta ya elimu kuanzia Sera,Miongozo na Mitaala yake ili kuleta mageuzi yenye tija.
“Mkutanu huu umekuja kipindi muafaka kwani dunia ipo katika mabadiliko na mageuzi makubwa katika sekta ya elimu ,hivyo sisi kama wadau tunapaswa kuisaidia serikali kufanikisha mageuzi haya kaa michango yetu ya mali na hali lengo likiwa ni kuendeleza sekta hii muhimu kwa taifa,” Amesema Faith
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja