November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkataba wa DP World, Serikali waanikwa

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

KAMPUNI ya DP World imesaini mkataba wa miaka 30 na Serikali ya
Tanzania kuendesha na kuboresha maeneo mahususi ya Bandari
ya Dar es Salaam, na kuiunganisha Tanzania na masoko makubwa duniani.

Mkataba huo wa uendeshaji umetiwa saini jana Ikulu ya Chamwino, jijini
Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari za Tanzania (TPA),
Plasduce Mbossa, na Sultan Ahmed Bin Sulayem, Mwenyekiti na Mtendaji
Mkuu wa Kampuni Tanzu za DP World, mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Mikataba hiyo unaainisha maeneo mahususi ya uwekezaji, mkataba huu wa
uendeshaji na uboreshaji unalenga kuongeza ufanisi wa bandari ya Dar
es Salaam kwenye usafirishaji na uchukuzi wa mizigo inayoingia na
kutoka nchini Tanzania.

DP World itaanza kwa kuwekeza dola milioni 250 kuboresha bandari, na
uwekezaji unatarajiwa kufikia dola bilioni moja, ikiwa ni pamoja na
uendelezaji wa maeneo mengine ya shughuli za bandari.

Uwekezaji huu utakuwa na faida kubwa kwa Tanzania hasa katika maeneo
muhimu kama vile kutengeneza ajira na kuongeza urahisi wa kupata
huduma na bidhaa, pamoja na mambo mengine.

Kwa uwekezaji huu, bandari ya Dar es Salaam itaunganishwa na maeneo
mengine ya mbali kwenye eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa
kutumia mtandao wa barabara, reli, njia kuu za kupitisha mizigo (logistics corridors) na bandari nyingine, na hivyo kusaidia sana kupunguza pengo la mahitaji ya huduma za uchukuzi barani Afrika
na kuunganisha biashara za eneo hili na masoko ya dunia.

Kupitia mkataba huo wa uendeshaji, DP World itakodishwa gati namba
4-7, na kuruhusiwa kutoa huduma kwenye gati namba 0-3 katika bandari
ya Dar es Salaam.

Uwekezaji huu mpya utaimarisha zaidi bandari hiyo ambayo katika miaka
ya karibuni ilinufaika na jitihada za serikali ya Tanzania kuboresha bandari zake.

DP World itafanya kazi na TPA na wadau wengine wa bandari kuhakikisha
kasi ya uondoaji wa mizigo bandarini inaongezeka na kwa utaratibu wa
kisasa – ikizingatia upekee wa bandari ya Dar es Salaam kama lango muhimu la usafirishaji (kwa njia ya maji) wa madini ya shaba kutoka Afrika ya Kati na Kusini kwenda kwenye masoko ya kimataifa.

Kuongezeka kwa ufanisi kutavutia meli nyingi na kubwa zaidi kutumia bandari ya Dar es Salaam; jambo litakalopunguza gharama kwa waagizaji na wasafirishaji wanaotumia bandari hiyo.

Vilevile, DP World itawekeza kwenye miundombinu ya kisasa kwenye bandari hiyo, ikiwemo uwekaji wa majokofu ili kusaidia wakulima na wafanyabiashara ya mbogamboga na matunda kuhifadhi bidhaa zao zisiharibike kabla ya kusafirishwa.

Zaidi ya hapo uwekezaji utaongeza urahisi wa kufikika kwa maeneo yanayotumia reli na yale yatakayotengwa kama maeneo ya
uwekezaji ili kuboresha miundombinu na kuongeza ushawishi wa Tanzania kuvutia biashara duniani.

Akizungumza katika utiaji saini huo, Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa
Kampuni Tanzu za DP World, Sultan Ahmed Bin Sulayem, amesema:
“Ni heshima kubwa kwetu kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuiboresha Bandari ya Dar es Salaam. Hatua hii inaendana na mipango ya kimkakati ya maendeleo inayopangwa na Tanzania na ni uthibitisho wa uongozi mahiri wenye maono wa Rais
Samia Suluhu Hassan.

“Jambo hili litatoa fursa nyingi kwa eneo hili la Afrika kwa kuliunganisha na masoko ya dunia, kutengeneza ajira nyingi zaidi,
kuongeza upatikanaji wa huduma na bidhaa, na kuongeza tija kwa wadau
wote.

Mkataba huu ni mwendelezo wa dhamira ya DP World kuunganisha watu na biashara kwa lengo la kukuza uchumi wa dunia. Pamoja na bandari nyingine tunazofanya nazo kazi, uwekezaji huu ni hatua
nyingine kwenye jitihada zetu pana za kushirikisha wataalamu wetu wa kimataifa na wazawa wa nchi husika kukuza mnyororo wa usafirishaji ili kukuza uchumi wa bara zima la Afrika”.

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema: “Kusainiwa kwa
mkataba huu baina ya Serikali ya Tanzania na DP World ni tukio kubwa
kwa sababu unatupa uwezo wa kujenga miundombinu ya kisasa kwa kutumia
ushirikiano baina ya serikali na sekta binafsi.

Kwa kutumia utaalamu wa DP World, bandari hii itakuwa chachu ya kusababisha kupatikana kwa ajira za moja kwa moja na nyingine kupitia sekta kama vile usafirishaji, usambazaji na mnyororo mzima wa sekta hii. Kikubwa zaidi,

Mamlaka ya Bandari (TPA) itamiliki hisa kwenye kampuni itayotekeleza
uwekezaji huu bandarini, na hakutakuwa na ajira yoyote itakayopotea.”

Akizungumza katika tukio hilo Mkurugenzi Mkuu TPA, Mbossa, amesema:
“Tuna furaha kubwa kushirikiana na DP World kwenye uboreshaji wa bandari ya kimkakati ya Dar es Salaam. Mradi huu
utaongeza tija kwa watumiaji na kuisaidia serikali katika lengo lake la kupunguza gharama za usafirishaji.

Mradi huu wa kimkakati ni ushahidi wa uwezo wetu wa kutekeleza miradi mikubwa ya miundombinu kwa kushirikiana na wabia wetu, na hivyo kuipa
serikali nguvu ya kutumia fedha zake kwenye sekta nyingine zenye
uhitaji zaidi”.

DP World inaendelea kufanya uwekezaji mkubwa kufikia malengo yake ya
kimkakati barani Afrika yanayolenga kukuza uchumi na kuboresha maisha
ya wananchi kwa kuwezesha biashara na kuunganisha masoko kwenye mtandao wa dunia.