January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkalama waomba kipaumbele cha mgao wa walimu

Na Joyce Kasiki,Dodoma

MBUNGE wa Iramba Mashariki Francis Mtinga (CCM)  ameiomba Serikali kuipa kipaumbele halmashauri ya wilaya ya Mkalama katika mgao ujao wa walimu  kutokana na upungufu uliopo.

Akiuliza swali la nyongeza Bungeni Feb 8,2024 Mbunge huyo pia aliitaka kujua mpango wa haraka wa Serikali wa kuziba majengo ya watumishi hao wanaostaafu au kufariki badala ya kusubiri ajira mpya.

“Kwa kuwa watumishi wetu wa umma wale wanaofariki na kustaafu tayari wanakuwa kwenye ikama ya serikali ,je serikali ina mpango gani wa haraka wa kuziba mapengo yote yanayoachwa na watumishi hao badala ya kusubiri ajira zinazotangazwa na Rais?alihoji Mtinga

Katika swali la msingi Mbunge huyo aliitaka kujua kama serikali  inafahamu kuna upungufu wa walimu kiasi gani katika halmashauri ya ya Mkalama na kama ina mpango wowote wa kupunguza pengo hilo.

“Je, Serikali inafahamu kuna upungufu kiasi gani wa Walimu katika Halmashauri ya Mkalama na ina mpango gani kupunguza pengo hili.?”

Akijibu maswali hayo Naibu waziri Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Deo Ndejembi amesema Serikali ipo mbioni kuajiri ajira mpya za walimu ambazo hivi karibuni zitatangazwa.

“Na  baada ya mchakato huo kukamilika serikali itaweka kipaumbele katika maeneo ya pembezoni ikiwemo halmashauri ya wilaya ya Mkalama.”amesema Ndejembi

Kuhusu kuziba mapengo ya watumishi wanaofariki na wanaostaafu Ndejembi amesema mshahara unakuwa katika bajeti ya mwaka husika hivyo mwajiri  aklichelewa kuomba kibali cha ajira mbadala ule mshahara unakuwa haupo katika mwaka unaofuata.

“Kwa hiyo niwatake waajiri pale wanapopata kifo au kuhama waombe vibali vya ajira mbadala mara moja ili sisi tuweze kuyaweka pamoja maombi yale na kuyapeleka utumishi ili kupata vibali vya ajira mbadala ndani ya mwaka wa fedha husika.” Amesisitiza Ndejembi

Kuhusu upungufu wa walimu halmashauri ya wilaya ya Mkalama amesema  mwaka 2022 Serikali iliajiri Walimu 9,800 nchi nzima na halmashauri ya Wilaya ya Mkalama ilipangiwa walimu ajira mpya 70 kati ya hao walimu 52 wa shule za msingi na 18 kwa shule za sekondari ambapo mwaka 2023 Serikali iliajiri walimu 13,130 na Halmashauri ya Mkalama ilipangiwa Walimu 92; kati yao walimu hao, 65 kwa shule za Msingi na 27 kwa shule za Sekondari.

Aidha Ndejembi amesema  Serikali inatambua mahitaji ya Walimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama na maeneo mengine na kwamba Serikali itaendelea kuajiri walimu kadri ya upatikanaji wa fedha.