January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

MJNUAT kuanza rasmi kutoa mafunzo mwaka huu ,Prof.Mkenda aagiza kukamilishwa kwa matayarisho yote

Na WyEST,Butiama-Mara

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda amekitaka Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT) kilichopo Butiama mkoani Mara kujikita kutoa mafunzo kwenye eneo la kilimo kwa upana wake ambao ndio msingi halisi wa uanzishwaji wa chuo hicho.

Prof. Mkenda ameyasema hayo Wilayani Butiama alipotembelea  chuo hicho na kuwataka kuhakikisha kuwa pamoja na mafunzo wanafanya tafiti  na kusambaza matokeo ya tafiti hizo ili kunuifaisha wakulima kwa kuongeza tija na uzalishaji.

Waziri Mkenda ameeleza kuwa chuo hicho kitaanza rasmi kutoa mafunzo mwaka huu 2023 na kuagiza uongozi wa chuo  kuhakikisha matayarisho yote yanakamilika.

Amesema mikakati  mbalimbali itatumika kuhakikisha wanafikia vigezo vya kupata ithibati ili kuruhusu kutoa mafunzo ikiwemo kuongeza wanataaluma na kuweka mazingira na miundombinu stahiki ya kufundishia na kujifunzia. 

“Tutahakikisha  MJNUAT Butiama kinaanza kutoa Mafunzo mwaka huu 2023, tayari Serikali imetoa Shilingi bilioni 2.6 kwa ajili ya kukarabati  majengo yaliyopo na kujenga hosteli mpya 2 ili wanafunzi watakapoingia wakae katika mazingira bora,” amefafanua Waziri Mkenda.

Profesa Mkenda ameongeza kuwa Serikali pia imetenga kiasi cha Shilingi bilioni 102 kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) kwa ajili ya kujenga makao makuu ya Chuo hicho hapo hapo Butiama.

Amesisitiza kuwa uwepo wa MJNUAT ni moja ya njia za kuenzi maono ya Baba wa Taifa kuhusu kutoa elimu ujuzi ikiwemo elimu ya kilimo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Mhe. Mosses Kaegele ameishukuru Serikali kwa kuendeleza Ujenzi wa Chuo Kikuu cha MJNUAT na kuhakikisha kinakwenda kuanza kutoa mafunzo mwaka huu. 

“Tunapongeza sana kwa hatua hii ya Wizara kuhakikisha Chuo kinaanza udahili . Na katika kazi ya ukarabati Mhe. katika Wilaya tuna uzoefu na kazi za ujenzi kupitia mfumo wa Force account, tutasaidia  kuhakikisha kazi inafanyika kwa ubora ili thamani ya pesa  ionekane,” ameongeza Mhe. Kaegele.

kwa upande wake Mbunge wa Butiama Jumanne Sagini ameipongeza Wizara ya Elimu kwa kutoa fedha kukiendeleza Chuo cha MJNUAT kuhakikisha  sasa kinakwenda kuanza kutoa mafunzo, kuunda Baraza, kuteua Mwenyekiti na Mkuu wa Chuo.

“Napongeza pia mtazamo wa Wizara kuhusu mafunzo kuhakikisha yanajenga ujuzi. Hii inaashiria kuwa vijana wakitoka hapo  MJNUAT wataweza kujiajiri katika kilimo,” ameongeza Sagini.

Kwa upande wake Kaimu Makamu Mkuu wa chuo cha MJNUAT, Prof. Lesakit Mellau amesema chuo hicho kinaendeshwa kwa usajili wa muda ‘provisional registration license’ na kwamba kilianza rasmi Machi 2015 baada ya Rais wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Kikwete kuteua viongozi.

Amesema kuwa tayari wameshaandaa mitaala 29 ikiwemo 20 ya Shahada ya Awali na 9 ya Diploma na kuongeza kuwa udahili unaotarajia kuanza baadae mwaka huu utaanza na wanafunzi 400.