Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Korogwe
MJI wa Lushoto na viunga vyake, unatarajiwa kuongezeka huduma ya majisafi na salama kutoka lita milioni 2,288,838 kwa siku hadi lita milioni 2,720,838 kwa siku, mara baada ya Mrad wa Maji Kwesimu utakapokamilika.
Maeneo yatakayonufaika na mradi huo ni Mji wa Lushoto, Kitopeni, Jegestali, Magereza, Hazina, Mabwawani na Chakechake, na wananchi 5,427 watanufaika na mradi huo.
Hayo yalisemwa (Juni 4, 2022) na Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Lushoto Mhandisi Erwin Sizinga kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Sahili Geraruma alipotembelea kuweka jiwe la msingi kwenye Mradi wa Maji Kwesimu ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 95.
Mradi huo ulioanza Februari mosi, mwaka huu na huku ukitarajiwa kukamilika Juni 30, mwaka huu, unatarajiwa kuzalisha lita 432,000 za maji kwa siku, huku ukigharimu sh. milioni 250,782,690, ambapo kati ya fedha hizo, sh. milioni 134,416,632 ni gharama za mkandarasi za utekekezaji wa mradi.
Na sh. milioni 116,365,690, ni gharama za mkataba wa ununuzi wa bomba uliofungwa na RUWASA Makao Makuu Dodoma, na hadi sasa mkandarasi M/S Yire Ladder Company Limited ya jijini Dar es Salaam, amelipwa sh. milioni 98,219,513 kwenye mkataba wake kama malipo ya awali (Advance Payment).
“Kazi zilizofanyika ni pamoja na ujenzi wa chanzo kipya cha maji, ufyekaji wa njia ya bomba, uchimbaji wa mitaro katika njia kuu ya bomba yenye urefu wa mita 3,000, uchimbaji wa mitaro njia za mitawanyo zenye urefu wa mita 200, ufungaji wa bomba katika njia kuu na njia za mitawanyo za bomba zenye urefu wa mita 3,200.
“Ujenzi wa vyumba vali viwili (Air valve), ujenzi wa visafishio viwili (Wash out) na ufungaji wa flow meter mbili. Utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 95, na unategemewa kukamilika Juni 30, 2022 ili uweze kuhudumia wananchi wa Lushoto” alisema Sizinga.
Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Kalisti Lazaro alisema Wilaya ya Lushoto yenye Halmashauri mbili, Lushoto na Bumbuli, jumla ya miradi 11 yenye thamani ya sh. bilioni 3.46 ilitembelewa na Mwenge wa Uhuru.
Mradi wa Maji Kwesimu, ni moja ya miradi inayotekelezwa nchi nzima kwa fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Usawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19, na kutekekezwa na Ofisi ya RUWASA Wilaya ya Lushoto.
More Stories
Kapinga asema mafanikio katika sekta ya nishati yanatokana na jitihada za Rais Samia
Bumbuli kutekeleza miradi kwa kuangalia vipaumbele
Makalla:Kupanga fujo ni dalili za kushindwa uchaguzi