December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mji wa Korogwe kuongezewa upatikanaji maji

Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Korogwe

WANANCHI wa mitaa ya Mbeza, Mtonga, Kwamkole na Memba katika Halmashauri ya Mji Korogwe mkoani Tanga, wataondokana na kero ya kukosa huduma ya maji safi mara baada ya mradi wa ukarabati wa chanzo cha maji kutoka Mbeza hadi tanki la Kwamkole utakapokamilika.

Akizungumza mbele ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Sahili Geraruma, alipotembelea mradi huo Juni 5, 2022, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Korogwe (KUWASA) Mhandisi Sifael Masawa, alisema mradi huo ukikamilika utahudumia wananchi 13,528.

“Mradi wa ukarabati wa bomba kutoka chanzo cha Mbeza hadi tanki la Kwamkole unahusisha uchimbaji na ulazaji wa bomba lenye kipenyo cha nchi sita, urefu wa kilomita 6.4 na ujenzi wa “valve chamber” sita, ambapo chanzo cha maji ni kijito cha Mbeza. Mradi huu unatekelezwa baada ya bomba la awali kupunguza uwezo wake wa kupitisha maji kwa kuwa chakavu, ambalo lilijengwa mwaka 1956.

“Mradi huu ukikamilika utahudumia wananchi wapatao 13,528 katika maeneo ya Mbeza Mtonga Kwamkole na Memba katika Halmashauri ya Mji Korogwe. Pia mradi huu umetoa ajira kwa wananchi, ambapo wanawake walikuwa 16 na wanaume 57 na kufanya jumla ya ajira kuwa 73” alisema Mhandisi Masawa.

Mhandisi Masawa alisema mradi huo unatekelezwa na mkandarasi Saxon Building Contractors Ltd kwa upande wa uchimbaji wa mtaro na ulazaji wa bomba na ujenzi wa chemba za valvu. Vifaa vimenunuliwa kwa wazabuni tofauti tofauti ambapo Lake Pipes Ltd amewauzia mabomba.

Ligera General Supplies amewauzia viungio vya mabomba, na Tanzania Steel Pipes amewauzia bomba za chuma. Ujenzi wa mradi huo unagharimu kiasi cha sh. milioni 498,852,953, na kiasi cha sh. milioni 445,611,448 kimetumika ikiwa ni malipo ya wazabuni na mkandarasi, na hadi sasa mradi umekamilika kwa asilimia 96

Alisema utekelezaji wa mradi huo ni wa fedha za UVIKO 19, na wanaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, kwani mradi huo utapunguza kero kwa kiasi kikubwa kwa wananchi.

Bomba la maji katika Mradi wa ukarabati wa chanzo cha maji kutoka Mbeza. (Picha na Yusuph Mussa).