January 4, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mizinga 300 ya kisasa yatolewa kupambana na ujangili, kuongeza uzalishaji wa asali

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

SERIKALI kupitia Mradi wa Kupambana na Ujangili na Biashara Haramu ya Wanyamapori (IWT) chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, imekabidhi mizinga ya kisasa 300 pamoja na vifaa vya kufugia nyuki na kusindika asali vyenye thamani ya shilingi milioni 50 kwa Jumuiya za Hifadhi ya Wanyamapori (WAGA) katika hafla iliyofanyika leo, Wilaya ya Mafinga, mkoani Iringa.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana alisema kuwa mizinga hiyo itasaidia kuimarisha uzalishaji wa asali nchini, ikiwa WAGA watatumia vizuri mafunzo na vifaa hivyo. “Mizinga hii inaweza kuzalisha wastani wa tani 10 za asali zenye thamani ya shilingi milioni 150 kwa mwaka endapo itatumiwa ipasavyo,” alisema Waziri Chana.

Aidha, Waziri Chana alihimiza Jumuiya ya WAGA kuhakikisha inatunza vizuri mizinga hiyo ili kuleta matokeo chanya kwa faida ya jamii na taifa kwa ujumla.

Katika hatua nyingine, Chana alibainisha kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii imeanzisha Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Ufugaji Nyuki, ambao unalenga kuwezesha vijana na wanawake kujihusisha na uzalishaji na biashara ya mazao ya nyuki. Mpango huo unatarajiwa kuongeza uzalishaji wa asali nchini kutoka tani 32,000 hadi tani 185,379 kwa mwaka, huku kiwango cha asali kinachouzwa nje ya nchi kikiongezeka kutoka asilimia 5 hadi 30, na mapato ya fedha za kigeni kutoka dola milioni 8 hadi dola milioni 20 kwa mwaka.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki wa Wizara hiyo, Deusdedit Bwoyo, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, alisema makabidhiano ya mizinga hiyo ni sehemu ya mkakati wa kuwezesha jamii zinazozunguka hifadhi kwenye mfumo wa ikolojia ya Ruaha – Rungwa kujikimu, ili kupunguza utegemezi kwenye maliasili.

Bwoyo aliongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025, mradi huo utasaidia miradi mingine ya ufugaji nyuki na kilimo yenye thamani ya shilingi milioni 337 kwa vikundi 21 katika wilaya za Itigi, Mbarali, na Mufindi.

Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi wa Chama na Serikali, wadau wa sekta ya nyuki, na watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii.