Na Martha Fatael, TimesMajira Online
ZAIDI ya wadau 150 wa sekta ya habari wakiwemo wahariri na waandishi wa habari wanatarajiwa kukutana Mkoani Iringa kesho Machi 17, 2026 katika kongamano maalumu litakalojadili nafasi ya vyombo vya habari katika kutangaza na kuibua fursa za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Kongamano hilo lililoandaliwa na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika – Tawi la Tanzania (MISA Tanzania) litafanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa na linatarajiwa kuwakutanisha washiriki kutoka Tanzania Bara na Visiwani.

Mwenyekiti wa MISA Tanzania, Edwin Soko amesema kongamano hilo linajulikana kama MISA Wadau Summit 2026 na linalenga kujadili namna ambavyo vyombo vya habari vinaweza kusaidia kutangaza fursa mbalimbali za maendeleo zilizopo mkoani Iringa.
Amesema mkutano huo utamkutanisha mgeni rasmi ambaye ni mkuu wa mkoa wa Iringa, Kheri James pamoja na wadau kutoka serikalini, sekta binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali ili kujadili mchango wa vyombo vya habari katika kuibua na kuendeleza fursa za kiuchumi.
Kwa mujibu wa Soko, kongamano hilo pia litatoa nafasi kwa wataalamu kutoka serikali ya mkoa huo pamoja na taasisi mbalimbali kuwasilisha mada zitakazoelezea mwelekeo wa mkoa huo katika kuibua na kuendeleza fursa za uwekezaji, utalii na maendeleo ya jamii.

Ametaja baadhi ya taasisi zitakazotoa mada kuwa ni pamoja na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Mfuko wa Taifa wa Sayansi na Teknolojia (NeST) na Magnina Print, akisema mada hizo zinalenga kuwajengea uwezo waandishi wa habari pamoja na kuwafungua kwenye fursa zilizopo katika sekta mbalimbali.
Soko amesema kauli mbiu ya kongamano la mwaka huu imechukuliwa kutoka mkoa wa Iringa inayosema “Iringa Imara Tutaijenga kwa Umoja na Uwajibikaji,” ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wa uongozi wa mkoa huo katika kusukuma agenda za maendeleo.
Hata hivyo ameongeza kuwa siku ya pili ya kongamano hilo Machi 18, wahariri na waandishi wa habari watapata fursa ya kutembelea hifadhi ya taifa ya Ruaha ili kujionea vivutio vya utalii na rasilimali za asili, hatua itakayosaidia kuwajengea uwezo wa kuwa mabalozi wa kuitangaza Iringa na Tanzania kwa ujumla.


More Stories
FIFA na TFF yaanza utambuzi wa vipaji vya Watoto mkoani Rukwa
JAI yapanga kulisha wagonjwa zaidi ya 1,800 Eid El-Fitr, yafanya hafla ya uchangishaji
Sema na Waziri kutatua changamoto za kisheria kwa wananchi