December 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Miradi ya Boost ya Bil 1.9 yatekelezwa Manispaa Tabora

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

HALMASHAURI ya manispaa Tabora imefanikiwa kuboresha miundombinu ya shule za msingi iliyokuwa imechakaa, kujenga vyumba vipya vya madarasa ya kisasa, matundu ya vyoo, majengo ya utawala na shule mpya kwa zaidi ya sh bil 1.89 za mradi wa boost.

Hayo yamebainishwa jana na Kaimu Afisa Elimu Msingi wa halmashauri hiyo Felisiana Muyaga alipokuwa akitoa taarifa kwa waandishi wa habari ambapo amebainisha kuwa fedha hizo zimefanya shule za msingi kuwa na mazingira bora zaidi ya kusomea.

Amefafanua kuwa fedha hizo zimejenga jumla ya vyumba 55 vya madarasa ya kisasa, majengo 3 ya utawala na matundu 82 ya vyoo bora katika shule mbalimbali za msingi, ikiwemo ujenzi wa shule mpya ya msingi Kidatu yenye mikondo 2 iliyogharimu zaidi ya sh mil.560.

Miradi mingine ni ukarabati wa shule ya msingi Mabatini uliogharimu zaidi ya mil 360 na ujenzi wa vyumba 4 vya madarasa katika shule ya Izenga, vyumba 3 Majengo, vyumba 3 Kalunde, vyumba 2 Kizigo, vyumba 2 Chemchem na ununuzi wa madawati 825 na samani nyingine za madarasa hayo.

Muyaga ameongeza kuwa pia wamepokea zaidi ya sh mil 380 kutoka serikali kuu kwa ajili ya kuifanyia ukarabati mkubwa shule kongwe ya Mabatini ikiwemo ujenzi wa vyumba 9 vya madarasa kwa gharama ya sh mil 180 na sh mil 37.5 za umaliziaji maboma 3 ya shule ya msingi Izenga

Kazi nyingine zilizofanyika ni ujenzi wa vyumba 3 Ifucha kwa gharama ya sh mil 37.5, vyumba 3 Mtongi kwa sh mil 37.5, vyumba 2 Kalunde kwa sh mil 25 na chumba 1 Kabila kwa gharama ya sh mil 12.5.

Kwa upande wa vyoo amesema matundu 12 yamejengwa katika shule ya msingi Usule kwa sh mil 13.2, matundu 8 Farm Nyamwezi kwa mil 8.8, matundu 8 Timkeni kwa sh mil 8.8, matundu 8 Igombe B (Mwibiti) sh mil 8.8, matundu 8 Mtongi sh mil 8.8 na matundu 6 Hengele kwa sh mil 6.6.

Amebainisha kuwa asilimia 99.9 ya miradi hiyo imekamilika na iliyobaki ipo katika hatua ya umaliziaji ili kuanza kutumika mwezi huu wa Januari mara tu baada ya shule kufunguliwa.

Amemshukuru Rais wa awamu ya 6 Dkt Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake kubwa za kuboresha miundombinu ya sekta ya elimu nchini, na kuongeza kuwa maboresho hayo yataongeza mahudhurio na kuchochea kwa kiasi kikubwa ufaulu mzuri wa watoto wote wa manispaa hiyo.