Na Mwandishi Wetu, TimesMajira online,Arusha
SERIKALI kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS),Mkoa wa Arusha,imekamilisha miradi ya kitaifa ya ujenzi wa barabara zenye urefu wa km 82.5 kwa kiwango cha lami kwa gharama ya sh. bilioni 189.141.
Miradi hiyo ya barabara ya Sakina-Tengeru (njia nne) km 14.1, barabara ya mchepuko wa Kusini (Arusha Bypass) Km 42.4 na ujenzi wa barabara ya Kia hadi Mererani na zote zimekamilika kwa asilimia mia moja.
Akitoa taarifa ya miradi hiyo jana kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, Meneja wa TANROADS mkoani Arusha,Mhandisi Johnny Kalupale, amemweleza kuwa, barabara ya Sakina hadi Tengeru (njia nne), yenye urefu wa km 14.1 imegharimu sh.bilioni 70.365, barabara ya mchepuko wa kusini ya urefu wa km 42.4, imejengwa kwa gharama ya sh. bilioni 86.778 huku barabara ya Kia hadi Mererani yenye urefu wa km 26 ikigharimu sh. bilioni 32.
Amesema wakala huo unaendelea na usimamizi wa miradi ya ujenzi wa barabara za Mto wa Mbu-Loliondo (km.49), Kijenge-Usariver (km 20) na ujenzi wa mzani wa kisasa wa kupima uzito wa magari katika eneo la Kimokouwa katika barabara ya Namanga pamoja na kuendeleza ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Sakina hadi Tengeru (km 9.3).
Akizungumza na watumishi wa TANROADS mkoani Arusha jana baada ya kukagua barabara hizo Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya,amewapongeza kwa kusimamia vyema miradi hiyo ya ujenzi wa barabara na kuhakikisha inakamilika kwa viwango vilivyoainishwa kwenye mikataba ya ujenzi, pia kuhakikisha barabara zote wanazozisimamia mkoani humo zinapitika majira yote ya mwaka.
“Nataka niwahakikishie kuwa,Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi yote ya uboreshaji wa miundombinu ya barabara iliyopo, lakini pia miradi mipya itakayotengewa fedha kwenye bajeti ya Serikali katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, nayo itatekelezwa,” amesema Mhandisi Kasekenya.
Naibu Waziri huyo alikuwa mkoani Arusha kwa ziara ya siku moja akitokea Dodoma kupitia barabara ya vumbi ya Kongwa kwenda Kibaya hadi Arusha (km 430), ambapo usanifu wa barabara hiyo umekamilika na ujenzi wake utatangazwa mara baada ya kutengewa fedha katika bajeti ya serikali kwa mwaka huu wa fedha
More Stories
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi
Rais Samia apongezwa kwa kuboresha huduma kwa wazee
Watu 5,000 kuhudhuria tamasha la utamaduni Songea