January 7, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Miradi maji kwa kutumia Force Account waleta tija

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Tunduru

IMEELEZWA kuwa ujenzi wa miradi ya maji kwa kutumia njia ya Force account katika maeneo mengi hapa nchini, umeleta tija kubwa na kupata miradi ya kiwango na ubora wa hali ya juu hivyo, serikali kutekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya kumtua mama ndoo kichwani na kuharakisha maendeleo ya wananchi.

Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugavi kutoka Wizara ya Maji, Dkt. Christopher Nditi alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mkowela Kata ya Namakambale Wilaya ya Tunduru, mara baada ya kukagua ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji hicho, unaotekelezwa na Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA).

Pia amesema mfumo wa Force Account, umesaidia kukoa fedha nyingi na kuwaongezea ujuzi wataalamu wa Wizara ya Maji, ili waweze kuwa na weledi katika kutekeleza na kusimamia miradi mbalimbali ya maji hapa nchini, badala ya kutumia wakandarasi ambao kwa muda mrefu wamekwamisha juhudi za wizara kufikisha huduma ya maji kwa wananchi.

Ameipongeza RUWASA ngazi ya wilaya na mkoa kwa kufanya kazi kwa pamoja wakati wote wa utekelezaji wa miradi, jambo lililowezesha miradi mingi ya maji katika Mkoa wa Ruvuma kukamilika kwa wakati na hivyo kuleta tija iliyokusudiwa na serikali ya kufikisha huduma ya maji kwenye makazi ya wananchi.

Kwa upande wake Meneja wa RUWASA Wilaya ya Tunduru, Primy Damas amesema mradi wa maji Mkowela umegharamiwa na Serikali Kuu kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji na kutekelezwa na RUWASA kwa kutumia njia ya lipa kutokana na matokeo (Force Account).