Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
IKIWA ni mwendelezo wa maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili Shirika lisilo la kiserikali la Mimi ni Taa Girls Foundation limefanya maadhimisho hayo kivingine kwa kuelimisha akina mama kuhusu masuala ya lisheili waweze kuwahudumia watoto vyema na kuwawezesha kufikia ukuaji timilifu.
Kwa maboresho yaliyoonekana kwenye taratibu za lishe kwa watoto wadogo ni pamoja na unyonyeshaji na lishe ya vyakula vya ziada kuwa ni sababu muhimu zilizochangia katika kupunguza kiwango cha udumavu kitaifa kutoka asilimia 34.7 mnamo mwaka 2015 hadi 2016 na kufikia asilimia 31.8 mwaka 2018.
Hata hivyo licha ya maboresho hayo ni muhimu kutambua kuwa udumavu mkali bado unaathiri mtoto mmoja kati ya watoto kumi nchini kote ,hii inamaanisha kwenye kila watoto kumi wa umri wa chini ya miaka mitano ,mtoto mmoja anaripotiwa kuwa na udumavu mkali ambapo inaashiria kwamba watoto milioni tatu walio chini ya umri wa miaka mitano nchini Tanzania wamedumaa.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo Mkurugenzi wa shirika hilo Dorcas Shayo amesema,shirika limeona lifanye hivyo kwani baadhi ya watoto wamekuwa wakikumbana na ukatili wa kukosa lishe bora na hivyo kupata utapiamlo na udumavu.
“Mwaka huu tumeona tufanye maadhimisho haya ya siku 16 za kupinga ukatili kivingine kwa kuelimisha akina kuhusu masuala ya lishe tukilenga kuzingatiwa kwa suala zima la lishe kwa watoto wadogo ili waweze kukua vyema.”amesema Dorcas na kuongeza kuwa
“Siku hizi akina mama wengi hawakai jikoni kwa ajili ya kuandaa vyakula vya watoto wao na kuhakikisha wanapata lishe bora (mlo kamili),kwa hiyo leo tumeona tutumie maadhimisho haya kutoa elimu kwa akina namna ya kuandaa mlo kamili kwa ajili ya watoto wadogo ambao pia unatumika hadi kwa watu wazima.”
Awali akizungumza na akina mama hao Mtaalam wa lishe kutoka shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na uhamasishaji wa masuala ya kilimo cha bustani za mbogamboga Mengo Chikoma amehimiza ulaji wa chakula unaofaa kwa maana ya kuzingatia makundi yote matano ya vyakula.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake aliyejitambulisha kwa jina la Josephine John mkazi wa Mailimbili jijini Dodoma aliyeshiriki maadhimisho hayo amesema,katika zoezi hilo la mapishi amejifunza kuwa jamii inapaswa kuendeleza kula vyakula vya asili kwani vingi ni kinga dhidi ya magonjwa mablimbali yakiwemo magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Vile vile amesema amejifunza namna ya kuandaa chakula cha mtoto mdogo chenye lishe bora ambacho ni kutoka katika makundi yote matano ya vyakula ili kusaidia watoto kukua vyema kimwili na kiakili na hivyo kuleta tija kwa Taifa hapo baadaye.
Kwa upande wake Afisa Lishe wa Jiji la Dodoma Semeni-Eva Juma amesema,Serikali kwa upande wake kupitia Maafisa Lishe wa Jiji la Dodoma imekuwa ikitoa elimu ya lishe kwa jamii ili washiriki vyema katika kupambana na udumavu katika jiji la Dodoma.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakani
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best