January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Milioni 420 yatekeleza miradi ya maendeleo Kata ya Kahama

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Miradi ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya milioni 420 imetekelezwa na Serikali ndani ya kata ya Kahama wilayani Ilemela mkoani Mwanza ikiwa ni jitihada za kuhakikisha wananchi wanapata huduma karibu na bora.

Akizungumza wakati wa kikao cha uwasilishaji wa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kipindi cha 2022/2023 kilichofanyika katika Kata hiyo Mtendaji wa Kata ya Kahama Victor Leonard, ameeleza kuwa serikali imejenga shule mpya ya sekondari ya Lubuka, shule mpya ya msingi Kahama.

Pia imejenga barabara, mitaro na madaraja Mtaa wa Magaka na Isela huku barabara ya kutoka Magaka na Kahama zikijengwa kwa kiwango cha Lami.

“Serikali iko na wananchi wake kuhakikisha miradi mikubwa na midogo ya maendeleo inatekelezwa,wanakahama tumepata fedha nyingi sana katika kipindi hiki kuliko kipindi chochote kwa ajili ya kufanya maendeleo,”ameeleza Victor.

Aidha ametumia fursa hiyo wananchi wa kata hiyo kuendelea kushirikiana na Serikali katika shughuli za maendeleo.

“Tunamshukuru Rais wa Samia Suluhu Hasan kwa kutoa fedha za maendeleo pamoja na Mbunge wetu Dkt.Angeline Mabula kwa namna anavyosimamia fedha hizo,”ameeleza.

Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kahama Mathayo Nicholaus Jibumbile mbali na kuipokea taarifa amepongeza utekelezaji wa maendeleo ndani ya kata yake pamoja na kuwataka wenyeviti wa mitaa kuhakikisha wanahamasisha jamii kupeleka watoto shule ili fedha za ujenzi wa madarasa zilizotolewa na Serikali ziwe na tija.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ata ya Kahama Samuel Shimbe,amewataka wananchi kuwa wavumilivu kutokana na kero ya ukosefu wa huduma ya uhakika ya maji.Kwani Serikali imeshachukua hatua kumaliza kero hiyo kwa kujenga tanki kubwa la maji jirani na ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Ilemela mradi uliogharimu zaidi ya bilioni sita mpaka kukamilika kwake.

Naye Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Ilemela Kanda ya Buswelu Julieth Peter amewataka wananchi kuhakikisha wanatumia fursa za kiuchumi zinazowazunguka ikiwemo mafunzo ya kilimo yanayotolewa na Serikali bila malipo na mikopo ya asilimia kumi ya mapato ya ndani inayotolewa na halmashauri zote nchini bila riba.

Mtendaji wa Kata ya Kahama Victor Leonard akiwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Ilani kwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Kata ya Kahama.
Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kahama Mathayo Nocholaus akizungumza katika wakati wa kikao cha kupokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya chama hicho kwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Kata ya Kahama.