Na Betty Kangonga,Timesmajira, Online
MILA na desturi za makabila mengi hapa nchini, zimechangia kwa kiasi kikubwa mwanamke kukosa haki ya kumiliki ardhi.
Kimila inadaiwa kuwa mwanamke umiliki ardhi kupitia kwa mume wake, mtoto wake wa kiume, au ndugu zake wa kiume. Hata hivyo, katika ngazi ya familia na ukoo.
Mwanamke ana haki ya kutumia ardhi kwa shughuli za uzalishaji kama vile kilimo na ufugaji. Kwasababu ya kutokuwa na umiliki wa ardhi, mwanamke amekuwa akikosa sauti katika mazao yatokanayo na ardhi aliyolima.
Mila na desturi zimempa mwanaume sauti na maamuzi katika ardhi. Wanawake wengi wamekuwa wakinyanyasika pindi wanapofiwa na waume au ndoa zinapovunjika.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 (kama ilivyofanyiwa marekebisho ya mara kwa mara) na Sheria za Ardhi zinatambua usawa na haki za mwanamke.
Ingawa matukio ya unyanyasaji wa mwanamke yamekuwa yakiendelea kila kukicha. Moja ya sababu ambazo zinachangia kuendelea kuwepo kwa matukio hayo ni uelewa mdogo wa jamii juu ya haki za mwanamke katika ardhi.
Kwa mujibu wa sheria za ardhi za mwaka 1999, ardhi yote Tanzania ni mali ya umma na iko chini ya usimamizi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano kama mdhamini kwa niaba ya wananchi wote.
Kabla ya kutungwa kwa sheria za ardhi mwaka 1999, sheria iliyotumika ilikuwa ni Sheria ya Ardhi namba 3 ya mwaka 1923.
Sheria hii ilitungwa wakati wa ukoloni na kutumika hadi mwezi Mei mwaka 2001 pale ambapo sheria mpya zilizotungwa mwaka 1999 zilipoanza kutumika. Hii sheria haikutambua na kulinda haki za mwanamke katika ardhi.
Bado hadi sasa kuna baadhi ya wanawake wanakabiliwa na changamoto ya kushindwa kumiliki ardhi hali inayochangia uwepo wa umaskini na kundi hilo kushindwa kujikwamua kiuchumi.
Baadhi ya wanawake katika kata ya Kisaki na Mngazi katika halmashauri ya Morogoro wanasema sababu zinazofanya kushindwa kumiliki ardhi ni ukosefu wa elimu, kutojua sheria za ardhi, hivyo kushindwa kuwa na maendeleleo na kuwa tegemezi ndani ya jamii.
Leah Patrick anasema, aliachika na kuachiwa watoto hivyo alilazimika kutafuta haki yake baada ya mumewe kuuza ardhi pasipo kumpatia sehemu yake na watoto.
Anasema kuwa alisimama kidete na kupambania haki kwa kupambana na wazee wa kimila na kuibuka mshindi.
Katika tukio lingine, Rosemary ambaye amebobea katika masuala ya haki za wanawake, alimsaidia mjane mmoja ambaye familia yake ilitaka kupora ardhi yake, kwa kuwasilisha shauri hilo katika Ofisi ya Mtendaji Kata, na kufanikiwa kurejeshewa shamba lake.
Naye Tatu Maleta wa Kijiji cha Gomero, Kata ya Kisaki ambaye ni mwangalizi wa masuala ya ardhi anasema kuwa bado elimu inahitajika zaidi ili kuwezesha wanawake wengi kuzijua haki zao na kuweza kumiliki ardhi.
Anasema kuwa amekuwa akiwashirikisha wanawake, vijana na wanaume kuhusiana na haki ya masuala ya ardhi ambapo kumekuwa na muitikio mkubwa miongoni mwa makundi hayo jambo linaloleta faraja kwao.
“Bado elimu inahitajika zaidi ili kuyafikia makundi mengi zaidi kwa kuwa hivi sasa wanawake wengi wanatambua haki zao na hata baadhi ya wanaume wameamka na kuanza kuandika kabisa wosia pasipo kuhofu jambo lolote,” anasema.
Anasema kuwa awali wengi walikuwa wakihofu kuandika wosia kwa kuona kama ni jambo la ‘uchuro’ na kujitabiria kifo lakini baada ya elimu wengi wao wameamka na kuwa tayari kuandika wosia ili kuepusha migogoro inayojitokeza pindi kinapotokea kifo.
Maleta anasema kuwa hata baadhi ya wajane baada ya kupata elimu wamefungua mirathi na kupata haki wanazostahili.
Anasema kuwa awali mfumo dume uliokuwa umejikita katika kijiji hicho ulisababisha wanawake wengi kupoteza haki zao za kumiliki ardhi ambapo ulianzia katika ngazi ya familia.
“Hivi sasa tumeamka elimu tunayopewa na mashirika mbalimbali yamesaidia kila mmoja kusimama ili kuhakikisha anapata haki ya kumiliki ardhi, anasema na kuongeza kuwa
…Yeye kama muangalizi wa masuala ya ardhi amekuwa akitoa elimu katika vikundi mbalimbali vya kijamii ikiwemo kanzisha maktaba katika makazi yake ili wananchi waweze kufika na kupata elimu ikiwemo kujua sheria na sera za masuala ya ardhi.”
Anasema kuwa kutokana na kupata hatimiki za kimila kupitia mkutano mkuu wa kijiji imesaidia wanaume kutambua kuwa wanawake wanauwezo mkubwa katika masuala mbalimbali.
“Elimu tuliyopata imetuwezesha hata kupata mikopo inayotolewa na Halmashauri na tunaweza kuendesha maisha yetu na kujiongezea kipato,” anasema.
Anasema kuwa ili kumuinua mwanamke kiuchumi lazima apate elimu ya kujitambua, kutambua fursa mbalimbali zinazomzunguka pamoja na kuwa na uelewa wa kisheria ili kuweza kujitetea pale ambapo tatizo limetokea na msaada wa kisheria anaotakiwa kupewa.
Winfrida anasema kuwa wanawake wengi wanashindwa kumiliki ardhi yao wenyewe kutokana na mila na desturi, kuna baadhi ya familia mwanamke haruhusiwi kumiliki mali ikiwemo ardhi hivyo huwafanya wanawake kutokuwa na sauti kwa jambo lolote ndani ya familia
Anasema kuwa elimu inayotolewa na wadau wa maendeleo kwa kushirikiana na serikali itasaidia kutatua changamoto zinazowakabili wanawake, kuwafanya kujiamini kuwa na sauti na kuweza na nguvu za kumiliki ardhi ili kuweza kujitegemea na kujikwamua kiuchumi.
Eutropia Kinoge anasema, wanawake wana majukumu mengi ndani ya familia, wanafanyiwa vitendo vingi vya ukatili wa kijinsia, wengi wanakuwa na uwoga kumiliki mali kwa kuhofia kuibiwa mali zao, kunyang’anywa na wanaume.
“Bado tunanyanyaswa ndani ya jamii, wanawake tunaongoza kufanyiwa vitendo ukatili wa kijinsia, naweza kulima mazao na mume wangu kipindi cha mavuno mwanaume anauza mazao yote na nikimuuliza ugomvi unaanza.” Anasema.
Kauli iliyowahi kutolewa na Mratibu wa Dawati la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Daniel Mallya anawataka wanawake kutumia fursa zilizopo kaika maeneo yao kujiendeleza na kuepuka kuwa tegemezi,na kuwataka kwa mujibu wa sheria ya ardhi namba 4 na namba 5,1999 mwanamke anapaswa kumiliki ardhi.
Mallya anasema inawasapa wanawake kujituma katika uzalishaji, kutumia elimu wanayopewa na wadau mbalimbali katika kuelimisha wanawake wengine ndani ya familia ili kuweza kuendelea na kuepuka kuwa tegemezi na kuweza kujitegemea wenyewe.
Moja ya kampeni iliyowahi kuzinduliwa hapa nchini inayojulikana kama kampeni ya ‘Linda ardhi ya mwanamke’ iliyoratibiwa na asasi za kiraia 26, inasema wanawake nchini wanashindwa kumiliki ardhi kutokana na mila na desturi kandamizi ambazo zinaonekana kuwa kikwazo kwao.
Hivyo uwepo wa kampeni hiyo itasaidia kuondoa fikra hizo potovu katika jamii.
Mwenyekiti wa kampeni hiyo, Tike Mwambipile anasema, lengo la kampeni hiyo ni kufunga ombwe lililopo kati ya sera au sheria na taratibu za maisha ya kila siku ya jamii za watanzania ikiwemo kubadili fikra za wanajamii kutoka katika mila kandamizi zinazozuia mwanamke kumiliki ardhi.
“Unaweza kwenda kijijini ukamwambia mwanamke kuwa unauwezo wa kumiliki ardhi akakataa kabisa na hiyo inatokana na mila na desturi tulizonazo ambazo nyingi zinamkandamiza mwanamke, ila naamini elimu ikitolewa wanawake watatuelewa.
“Na ndio maana tumekuja na kampeni hii ambayo italenga pia kuongeza nguvu ya haki ya wanawake kumiliki ardhi, kutoa maamuzi kuhusu ardhi na kufaidi mapato yatokanayo na ardhi,” anasema.
More Stories
Boost ilivyoboresha miundombinu ya elimu Ilemela
Samia apongeza walimu 5,000 kupatiwa mitungi ya gesi, majiko kutoka Oryx
Uwekezaji kwenye kilimo utatimiza ndoto ya Samia ya nchi kuwa ghala la chakula Afrika