Na Albano Midelo,TimesMajira online
SERIKALI mkoani Ruvuma imedhamiria kukuza sekta ya utalii na kuongeza idadi ya watalii wanaofika kutembelea vivutio lukuki vinavyopatikana ndani ya Mkoa.
Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Uchumi na Jamii(ESRF) Makao makuu jijini Dar es salaam Lunogelo Buhela akizungumza na wadau wa utalii mkoani Ruvuma ,anasema sekta hiyo kwa miaka mingi imekuwa inakabiliwa na changamoto mbalimbali.
Kwa mujibu wa Buhela Taasisi yake inashirikiana na wataalam katika Mkoa wa Ruvuma ili kutengeneza mpango mkakati wa kuendeleza sekta ya utalii katika Mkoa wa Ruvuma.
“Sekta ya utalii nchini Tanzania ni ya muhimu sana kiuchumi,utalii unaposhamiri una faida kubwa kwa serikali na watu binafsi,utafiti unaonesha kuwa Mkoa wa Ruvuma kwa miaka mingi umekuwa nyuma kuvuna fursa za utalii’’,anasema Buhela.
Kwa mujibu wa Mtafiti huyo Mwandamizi,katika watalii 300 wanaoingia Tanzania,Mkoa wa Ruvuma unapata mtalii mmoja tu jambo ambalo amesema limekuwa changamoto katika kukuza sekta ya utalii katika Mkoa huo.
Hata hivyo anasema Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa michache nchini yenye vivutio vya utalii vya aina mbalimbali na ambavyo havipatikani sehemu nyingine yeyote duniani .
Anavitaja miongoni mwa vivutio adimu katika Mkoa huo kuwa ni ziwa Nyasa ambalo ni kitovu cha utalii kutokana na kusheheni aina zote za vivutio vya utalii,vivutio vingine ni Hifadhi ya Taifa ya Nyerere,Makumbusho ya Taifa ya Majimaji,Mto Ruvuma, makanisa makongwe,ngoma za asili,utalii wa kilimo cha Ngoro, mapango na mawe ya kihistoria.
Anautaja mpango mkakati wa kukuza sekta ya utalii katika Mkoa wa Ruvuma unaweza kusaidia kuinua pato linalotokana na utalii ili kuchangia katika pato la Taifa na wananchi na kwamba watalii wanapoingia kwa wingi wanasisimua shughuli za kiuchumi kutokana na kulala,kunywa na kusafiri.
Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi wa Huduma za Uchumi na Uzalishaji Jeremiah Sendoro anasema mpango mkakati huo wa kukuza utalii utafanikiwa kwa sababu serikali imejitahidi kutatua changamoto zilizokuwa zinaikabili sekta ya utalii katika Mkoa wa Ruvuma.
Anabainisha zaidi kuwa serikali tayari imejenga miundombinu bora ya usafiri zikiwemo barabara za lami,meli katika ziwa Nyasa,kuboresha uwanja wa ndege wa Songea, kuanzisha safari za ndege za abiria na wawekezaji kujenga hoteli za kisasa katika Mkoa wa Ruvuma.
Afisa Maliasili na Utalii wa Mkoa wa Ruvuma Afrikanus Challe anasema ili mpango mkakati wa kukuza utalii upate matokeo chanya ni vema itolewe sera mpya ya utalii inayonufaisha mikoa ya kusini, elimu ya utalii iwe endelevu na matangazo ya kuvitangaza vivutio vya utalii mkoani Ruvuma yawe endelevu.
Challe anasema vivutio hivyo vikiendelezwa vinaweza kuchangia pato la Taifa na kuinua uchumi wa wananchi na kwamba karibu kila wilaya iliyopo katika mkoa wa Ruvuma ina vivutio mbalimbali vya utalii vinavyoweza kufungua milango ya utalii na kutoa ajira kwa vijana.
Hata hivyo Afisa Maliasili na Utalii wa Mkoa wa Ruvuma anashauri wadau wote katika maeneo husika zikiwemo Halmashauri,Wakala wa Barabara Mkoa TANROAD,Wakala wa Barabara wilaya TARURA,wamiliki wa hoteli, wafanyabiashara na wananchi wote kushirikiana ili kuongeza watalii watakaopenda kuwekeza na kutalii katika mkoa wa Ruvuma.
Challe anautaja mpango mkakati wa kukuza uchumi katika utalii mkoani Ruvuma kuwa ni kuwepo kwa njia kuu nne za kuingia watalii ambazo ni Madaba,Mkenda,Mbambabay na Tunduru.
“Watalii hawa huingia kutoka ndani ya nchi kupitia hifadhi ya Kitulo,Ruaha,Mikumi na Selous au toka nje ya nchi kama Msumbiji,Malawi,Zambia,Zimbabwe na Afrika ya Kusini nchi ambayo inaoongoza kwa utalii barani Afrika’’anasisitiza Challe.
Hata hivyo Challe anasema watalii wanaingia katika Mkoa wa Ruvuma kwa kiasi kidogo,kwa sababu ya kukosa mawasiliano na vituo vya taarifa za utalii vya mikoa jirani na nchi za jirani.
Anazitaja njia kuu mbili za kupita watalii toka nje ya mkoa wa Ruvuma hadi kwenye vituo vya utalii kuwa ni Njia ya Magharibi ambayo inapitia Mkenda-Liparamba-Tingi-Mbambabay-Liuli-Lundu-Lituhi-Litumbandyosi hadi Madaba.
Njia ya Mashariki anaitaja kuwa inaanzia Songea-Namtumbo-Likuyusekamaganga-Kalulu-Tunduru-Likumbule-Nalasi-Magazini-Lusewa hadi Songea na kwamba mkakati wa kukuza utalii katika mkoa wa Ruvuma unaonesha maeneo mapya muhimu ya uwekezaji wa hoteli za kitalii au camp site.
Afisa huyo wa Maliasili na Utalii anayataja maeneo hayo kuwa ni fukwe kando kando mwa ziwa Nyasa yakiwemo Mtupale hadi Lituhi,kijiji cha Chimate,Liuli,Lundu na Lituhi.
Maeneo mengine ni kando kando ya hifadhi yakiwemo kijiji cha Liparamba,Litumbandyosi,Kazamoyo,Muhuwesi,Ngapa,Likuyusekamaganga na Madaba.
Maeneo mengine ya uwekezaji yaliopo karibu na miji ya vivuko mpakani mwa Tanzania na Msumbiji anayataja kuwa ni Mkenda, Lukumbule na Magazini na makao makuu ya wilaya za Songea, Mbinga,Tunduru,Namtumbo na Mbambabay.
Hata hivyo Challe anasema sekta ya utalii katika Ukanda wa mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi inafanana kiikolojia na mikoa ya kaskazini ya nchi za Msumbiji,Afrika ya Kusini na Malawi.
Challe anabainisha kuwa licha ya mikoa hiyo kuwa na mahusiano mazuri ya kihistoria katika biashara ya utumwa ya kusini,vita ya wangoni na vita ya wapigania uhuru,bado aina hiyo ya utalii haijaendelezwa na kutangazwa.
Anasisitiza kuwa utalii huu wa kihistoria, kiutamaduni, kishujaa, utalii wa wanyamapori na mimea hauna uhusiano mzuri na haujatangazwa katika nchi hizo za kusini kwa kwamba baadhi ya maeneo hayana miundombinu ya uhakika kama barabara, madaraja,viwanja vya ndege na hoteli za kitalii.
Changamoto nyingine anaitaja kuwa ni uhaba mkubwa wa wafanyakazi wataalam,hakuna kampuni nyingi au Taasisi za kitalii(Tour Guide Operators) kama ilivyo katika mikoa ya Kaskazini ambayo ina kampuni nyingi zinazofanya kazi za kitalii ambazo zimetoa ajira kwa vijana.
Challe anaitaja mikakati ambayo inachukuliwa kuboresha sekta ya utalii katika mkoa wa Ruvuma ni kulinda wanyamapori kwa kushirikina na wananchi,kuufanya Mji wa Mbambabay wilayani Nyasa kuwa mji wa kitalii,kushirikisha sekta binafsi kwenye utalii na kuvitangaza vivutio vya utalii kwa wananchi.
Mikakati mingine ni kutengeneza mtandao wa wa kiutalii Kanda ya Kusini na kwamba kwa kuwa mkoa wa Ruvuma una dalili ya kupata watalii toka Afrika ya Kusini ni vema Balozi Tanzania nchini Afrika Kusini,kusaidia kuongeza matangazo ya vivutio vya mkoa wa Ruvuma.
Kwa ujumla mkoa wa Ruvuma bado una maliasili nyingi zikiwemo misitu,wanyamapori, samaki, mito, maziwa, milima, fukwe, mapango na rasilimali nyingine ambazo bado hazijaharibiwa hivyo zikiendelezwa zinaweza kutoa mchango mkubwa katika pato la Taifa na wananchi kupitia utalii.
More Stories
Ubunifu wa Rais Samia kupitia Royal Tour unavyozindi kunufaisha Tanzania
Rais Samia anavyojenga taasisi imara za haki jinai kukabilina na rushwa nchini
Rais Dk. Samia alivyowezesha Tanzania kuwa kinara usambazaji umeme Afrika