Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline,Songwe.
MADIWANI katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi kwa pamoja wameridhia na kupitisha pendekezo la kuvunjwa kwa Mamlaka za miji ya Vwawa na Mlowo ili kupata eneo moja la utawala litakalopandishwa hadhi na kuwa Halmashauri ya mji au Manispaa.
Azimio hilo limepitishwa Februari 14, 2024 katika kikao cha baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo, kilichoketi kujadili mambo mbaalimbali, ikiwemo ombi la kuridhia kuvunjwa kwa Mamlaka hizo mbili za miji ya Vwawa na Mlowo.
Awali Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Danny Tweve alitaja sababu za kuvunjwa kwa Mamlaka hizo mbili kuwa ni gharama kubwa za uendeshaji ikilinganishwa na kiwango cha ukusanyaji mapato katika Mamlaka hizo.
Tweve aliongeza kuwa mbali na gharama za uendeshaji wa Mamlaka hizo mbili kuwa kubwa pia maoni ya kamati ya Fedha, Utawala na mipango baada ya kujadili ilibaini kuwa kuendelea kuwa na Mamlaka za miji mbili ni mzigo mkubwa kwa Halmashauri ya Wilaya.
“Kwa sasa vigezo vya kupandishwa hadhi kuwa Halmashauri ya mji tunavyo, isipokuwa kuhusu manispaa bado hatujafikia vigezo kwa mujibu wa taratibu kwani moja ya kigezo kinachozingatiwa zaidi ni kuwa na uwezo wa kujiendesha kwa asilimia 30, jambo ambalo kwa sasa bado hatujafikia”amefafanua zaidi Tweve.
Wakijadili hoja hiyo ndani ya kikao hicho, madiwani hao kwa umoja wao warilidhia na kupitisha pendekezo hilo lililowasilishwa kikaoni hapo baada ya mchakato wa awali kufanyika katika vikao vya kamati ya Fedha, Utawala na mipango.
Mmoja wa madiwani hao, Aloyce Mdalavuma, amesema hakuna sababu ya kujadili na kuchukua muda mrefu kupitisha pendekezo hilo,kwa kuwa kufanya hivyo ni kuchelewesha maendeleo kwani wazo la Wilaya ya Mbozi kuwa na manispaa limechelewa sana.
“Mwenyekiti kinachotakiwa kufanyika kwa sasa si kujadili hoja hii kwa muda mrefu bali ni kupambana kama tulivyofanya wakati wa kupigania makao makuu ya mkoa kubaki hapa Vwawa, hivyo naomba kwa umoja wetu tupitishe pendekezo hili kwani ziko mbinu za mapambano za kuhakikisha tunapata Manispaa hata kama mnasema vigezo bado havijafika” alisisitiza Mdalavuma na kuungwa mkono na Madiwani wote huku wakipiga shangwe kwa kusema ‘imeisha hiyoo!’.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, George Msyani akihitimisha mjadala huo ndani ya kikao hicho cha baraza, , alisema pendekezo la kuvunjwa kwa mamlaka hizo mbili ni hatua za awali za mchakato wa kupata Halmashauri ya Mji na baadae kama sifa na vigezo zaidi vikipatikana hatimaye ipandishwe na kuwa Manispaa.
“kinachofanyika hivi sasa ni mchakato wa awali kwa mujibu wa taratibu na baada ya sisi kupitisha pendekezo hili, litapelekwa katika vikao vingine kama kamati za ushauri za maendleo za wilaya na mkoa (dcc na rcc) na baada ya hapo litafikishwa katika mamlaka za juu zaidi kwa ajili ya uamuzi”amesema msyani.
Akifafanua zaidi, mwenyekiti huyo wa halmashauri amesema baada ya mamlaka hizo za miji kuvunjwa na kuunganishwa kuwa sehemu moja ya utawala itaongeza sifa za kupandishwa hadhi kwa kuwa eneo hilo litakuwa na idadi ya wakazi wasiopungua laki moja.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu